TALGWU YALAANI MAUAJI YA MKUKI KWA MWANACHAMA WAKE


 Katibu Mkuu TALGWU Rashid Mtima akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro ( hawapo pichani)

Na Christina Cosmas, Morogoro


CHAMA cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa Tanzania (TALGWU) kimelaani mauaji ya mwanachama na kiongozi wao Madadi Omari Litumbui kwa kuchomwa mkuki na mfugaji wakati wakiwaondoa wafugaji katika msitu wa serikali uliounganisha vijiji na kuwa hifadhi moja Wilayani Kilwa Mkoani Lindi.

Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa Habari Katibu Mkuu wa TALGWU Rashid Mtima alisema tukio hilo lilitokea machi 17 mwaka huu wakati mtumishi huyo akiwa doria na wenzake ambapo alichomwa mkuki na kukimbizwa kituo cha afya Nanjilinji (Kilwa) na alifariki dunia usiku huohuo.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanachama na kiongozi wetu ndugu Medadi aliyekuwa mtendaji wa kijiji cha Mtumbei huku akihudumu TALGWU kwa nafasi ya Katibu wa kamati ya Uratibu Halmashari ya Wilaya ya Kilwa”, alisema.

Mtima alisema marehemu huyo alifariki dunia wakati akitekeleza majukumu yake kama mtendaji wa Kijiji cha Mtumbei Mpopela kata ya Kandawale Tarafa ya Kipatimu Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Hata hivyo aliiomba jeshi la polisi kuongeza nguvu ya kumtafuta mfugaji huyo wa jamii ya kimang’ati aliyemrushia mkuki mtumishi huyo na kumsababishia umauti.

“TALGWU inalaani vikali mauaji ya mwanachama wetu ndugu Medadi na itafuatilia kwa ukaribu kuhakikisha haki inatendeka, aidha tunaliomba Jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote waliohusika na mauaji hayo ya kinyama” alisema Mtima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post