PROF. MWEGOHA AONGOZA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI KUMUAGA MHADHIRI WA MZUMBE BALOZI DKT. KAMALA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William leo Februari 17, 2024 katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko - Dar es Salaam ameungana na ndugu, jamaa na marafiki, katika kuuaga mwili wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala aliyefariki dunia tarehe 12 Febuari 2024.


Prof. Mwegoha amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya – Othman, ambao kwa pamoja wamemwelezea Marehemu Balozi Kamala kama kiongozi aliyekuwa na maono ya kimkakati katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa ndani na nje ya nchi, kujenga amani na kuleta maendeleo kwa Tanzania kupitia nyadhifa mbalimbali alizoshika enzi za uhai wake.

“Tukio hili si jepesi kulipokea hasa ukizingatia mahusiano mema ambayo marehemu aliyejenga na wafanyakazi wenzake, wanafunzi na watu mbalimbali waliobahatika kukutana naye. Pia, ni pigo kubwa kwa jamii yetu na kwa nchi ya Tanzania kwa ujumla kupoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali hususan kwetu sisi wanataaluma” Amesisitiza Prof. Mwegoha

Amesema Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala atakumbukwa sana kwa mchango mkubwa kwa Chuo Kikuu Mzumbe toka alipokuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (IDM-Mzumbe), akiwa mtu aliyeipenda sana kazi yake katika kuongoza kundi kubwa la wanachuo na kuajiriwa kama Mkufunzi mwenye ufahamu wa hali juu katika masuala ya Uchumi.

“Mchango wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala bado unaishi na utaendelea kuishi kupitia kazi nyingi za kitaaluma na kisiasa alizozifanya. Moja ya vitu vinavyofariji ni sifa aliyokuwa nayo ya kupenda kuyaweka mawazo yake katika maandishi. Hii inatusaidia kubaki na rejea ya mambo aliyoyafahamu, vitu alivyoviamini na mawazo aliyoyajenga juu ya mambo mbalimbali” Amesisitiza Prof. Mwegoha.

Awali, Paroko wa Kanisa la Mwenyeheri Isidori Bakanja Padri Emmanuel Makusalo na Padri Florence Rutaihwa Rwehumbiza kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania walioendesha ibada ya misa ya mazishi, kwa pamoja, wamewataka waamini na waombolezaji kujiandaa na kifo kwa kudumu katika sala ili waweze kukikabili vema kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa.
nbsp;

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post