KINARA WA MTANDAO WA WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI AKAMATWA NA PUNDA WAKE DAR

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Bw. Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 25,2024 wakati akitoa taarifa baada ya kumkamata mfanyabiashara kinara wa dawa za kulevya ulimwenguni.
*******************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA,) imefanikiwa kumkamata kinara wa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina ya Cocaine nchini pamoja na gramu 692.336 za Cocaine.

Aina ya dawa hizo ambazo huzalishwa kwa wingi katika bara la Amerika Kusini na kusafirishwa kwa njia ya anga kupitia wabebaji (Punda,) ambao humeza dawa hizo tumboni au kuweka kwenye maungo ya mwili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Bw. Aretas Lyimo, amesema mfanyabiashara huyo (Mtanzania, jina limehifadhiwa,) aliyekuwa akitafutwa tangu mwaka 2000 ana mtandao mkubwa wa wabebaji dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali duniani ambao huwatumia kusafirisha dawa hizo kwa njia ya kumeza.

Amesema, Mfanyabiashara huyo kinara ambaye yupo mikononi mwa vyombo vya dola tayari kupelekwa mahakamani, alikamatwa katika eneo la Boko, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam akiwa na dawa za kulevya (Cocaine,) tayari kwa kuzisafirisha, amekuwa akitumia watu kumi kwa wiki kusafirisha dawa za kulevya ndani na nje ya nchi huku washirika wake wawili wakikamatwa katika Jiji la Dar es Salaam huku mmoja akikamatwa katika Kijiji cha Shamwengo Wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani Mbeya.

"Wabebaji wa dawa za kulevya maarufu kama Punda waliokuwa wanatumiwa na mfanyabiashara huyu wamekamatwa na kufungwa katika Nchi mbalimbali zikiwemo India, China na Msumbiji kupitia biashara hii, wengine hupoteza maisha baada ya dawa hizo kupasuka tumboni...Hii ni hatari watanzania tuungane kuwatokomeza watu hawa wanaowatumia watoto wa maskini kujipatia utajiri." amesema.

Akieleza namna dawa hizo zinazosafirishwa Kamishina Jenerali Lyimo amesema; vijana wadogo wasio na ajira wenye umri kati ya miaka 20- 35  na miaka 45 kwa uchache wamekuwa wakisafirisha dawa hizo ambazo zipo katika mfumo wa pipi kwa kumeza tumboni au kuweka katika maungo mengine ya mwili.

"Mtu mmoja hubeba kuanzia gramu 300 hadi 1200 na wengine hususani wenye matumbo makubwa hasa wanawake hubeba hadi gramu 2000 kwa wakati mmoja na hawa hupewa mafunzo ya kuhimili ubebaji huu ikiwemo kula vyakula vigumu, vingi ambavyo hutanua tumbo." Ameeleza.

Aidha amesema, Mamlaka hiyo itafanya operesheni kali za nchi kavu na baharini kwa mwaka 2024.

"Kwa upande wa nchi kavu zitahusisha mashamba ya dawa za kulevya, kwenye mipaka, maeneo ya mijini,  kwenye vijiwe vya usambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya....Kwa upande wa baharini operesheni hizo zitahusisha fukwe na katikati ya bahari" ,mefafanua.

Kwa watumiaji wa shisha, operesheni kali zitafanyika katika maeneo yote wanayouza na shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya na wote watakaobainika kutumia dawa za kulevya kupitia shisha watachuchukuliwa hatua za kisheria huku kampeni hiyo pia ikiwalenga wauzaji wanaokiuka taratibu za uuzaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu.

Kuhusiana na utekelezaji wa kampeni zinazoendelea dhidi ya magenge wa biashara hiyo haramu Kamishina Jenerali Lyimo ametoa onyo kwa wote watakaoendelea kujihusisha na uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini kuacha mara moja kwani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuiwezesha Mamlaka hiyo kwa kununua vifaa vya kisasa na mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka hiyo ili kuwajengea ujasiri na weledi katika kutekeleza operesheni kwa ufanisi mkubwa hivyo watakaoendelea na kilimo Cha bangi, mirungi na biashara ya dawa za kulevya viwandani watashughulikiwa ipasavyo.

"Tathmini inaonesha Mkoa wa Mara unaongoza kwa kilimo cha bangi baada ya Mkoa wa Arusha kupunguza uzalishaji huo...Tutapita katika Mikoa yote Tanga na Kilimanjaro ambako mirungi inazalishwa na mikoa yote ya Pwani pamoja na yote tuliyoifanyia na tusiyoifanyia ukaguzi na hakuna atakayebaki salama katika operesheni hii" ,amesema

Dawa ya kulevya aina ya Cocaine huzalishwa katika kutoka kwenye mmea wa Coca unaojulikana kitaalam kama Erythroxylum Coca (Coca Plant,) na hulimwa zaidi katika Nchi za Bolivia, Peru na Colombia zilizopo Amerika ya Kusini. Zikiwa katika kundi la dawa la vichangamshi huleta athari kubwa kwa mtumiaji ikiwemo kuathirika kwa mfumo wa fahamu, kukosa usingizi, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi, vifo vya ghafla, matatizo ya akili, hasira, vurugu, kukosa utulivu, mtumiaji kutaka kujiua pia husababisha uraibu wa haraka na utegemezi hivyo kuwa vigumu kwa mtumiaji kuiacha.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Aretas Lyimo akionesha namna mtandao wa wauzaji wa dawa kulevya wanatumia katika kusafirisha dawa hizo ulimwenguni. 
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Bw. Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 25,2024 wakati akitoa taarifa baada ya kumkamata mfanyabiashara kinara wa dawa za kulevya ulimwenguni.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Bw. Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 25,2024 wakati akitoa taarifa baada ya kumkamata mfanyabiashara kinara wa dawa za kulevya ulimwenguni.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post