WiLDAF YAFANYA MAFUNZO YA USAWA WA KIJINSIA KWA FORUM CC

  

Na Deogratius Temba, Dodoma

Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF),imefanya mafunzo ya kujenga uwezo kwa wafanyakazi wa Jukwaa la Mabadiliko ya tabia nchi (Forum CC), ili kuweza kuingiza masuala ya Kijinsia katika Programu na muundo wa shirika kwa ujumla. 

Mafunzo haya ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida) kupitia Save the Children-Tanzania, kwa lengo la kukuza uwezo wa asasi  za kiraia, kuimarisha mifumo ya kitaasisi na kuongeza sauti za watoto kujadili, kujisimamia  na kudai haki zao za msingi hasa katika eneo la Mabadiliko ya tabia nchi, unaotekelezwa kwa ushirikiano  na WILDAF, Forum CC na wadau wengine watano. 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Forum CC, Sarah Ngoy, amesema kwamba, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo mwaka jana 2022, taasisi hiyo ilifanya zoezi la kupima uwezo wake katika masuala ya Kijinsia na kuonekana kwamba kuna pengo kwenye eneo la usawa wa Kijinsia ndani ya taasisi. 

“Warsha hii kwa wafanyakazi wetu imekuja kwa wakati muafaka, mwaka jana tulipofanya zoezi la kujipima kama taasisi tuliona hili pengo la kijinsia ndani ya shirika, tukagundua kwamba pamoja na kuhitaji kujenga uwezo kwa wafanyakazi wetu kwenye masuala ya Kijinsia, ili kuzifanya program zetu ziwe na mtazamo wa Kijinsia, pia tulihitaji mabadiliko ya kimfumo,  sambamba na kuongeza uelewa na maarifa ya masuala ya kijinsia kwa timu yetu yote”, alisema Sarah  na kuongeza:

“Warsha hii imetufungua macho sana, kumbe bado tuna pengo la masuala ya kijinsia, kumbe tunahitaji kufanya mabadiliko na maboresho ya bajeti zetu ziweze kuwa na mtazamo wa kijinsia, kupitia mafunzo haya tumegundua kwamba tunatakiwa kuongeza mafunzo kwa wafanyakazi, kuweka bajeti kwaajili ya taulo za kike kwa wafanyakazi, kuweka chumba cha kupumzika mama wajawazito wanapokuwa ndani ya shirika letu, na pia kubadilisha mwongozo wa fedha ili kuruhusu kuwalipia gharama wasaidizi wa wanawake wanaonyonyesha na wasindikizaji wa watu wenye ulemavu” ,alisema Sarah. 

Ameongeza kwamba, mara baada ya mafunzo hayo, taasisi hiyo itakaa na kupitia upya sera za ndani ya shirika na miongozo mbalimbali ukiwemo ule wa rasilimali watu ili uweze kuendana  na sera ya Jinsia ya Taasisi sambamba na kuwa na mpango wa utekelezaji wa masuala ya Kijinsia kwa taasisi utakaoanza kutekelezwa mwaka 2024. 

Naye mwezeshaji kutoka WiLDAF, Deogratius Temba, amesema kwamba, WiLDAF ina matumaini kwamba, baada ya mafunzo hayo, mabadiliko makubwa ya kitaasisi yatatokea kwani washiriki wameweka ahadi (commitiment) ya kuweka nguvu kwenye mabadiliko ya kitaasisi ili  kila kitu kinachofanyika ndani ya shirika kiweze kuwa na mtazamo wa Kijinsia.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post