KAMPENI YA UHAMASISHAJI JAMII KUWA NA MTAZAMO CHANYA JUU YA HAKI YA AJIRA NA KUFANYA KAZI KWA VIJANA WENYE ULEMAVU NCHINI TANZANIA


Wakili Gidion Kaino Mandesi, Mkurugenzi Mtendaji wa DOLASED

 


KAMPENI YA UHAMASISHAJI JAMII KUWA NA MTAZAMO CHANYA JUU YA HAKI YA AJIRA NA KUFANYA KAZI KWA VIJANA WENYE ULEMAVU NCHINI TANZANIA

 

1. UTANGULIZI

      Shirika linaloshughulikia Masuala ya Kisheria, Maendeleo ya Jamii Na Uchumi Kwa Watu Wenye Ulemavu (DOLASED) kwa kushirikiana na shirika la Sightsavers, Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA), Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) na Shirika la Vijana wenye Ulemavu (YOWDO) wanafanya mradi wa pamoja wa kuwajengea uwezo kiuchumi Watu wenye Ulemavu nchini Tanzania (Tanzania Economic Empowerment Project).


     Uhamasishaji wa Jamii kuwa na mtizamo chanya juu ya haki ya ajira na kufanya kazi kwa vijana wenye ulemavu ni miongoni wa afua muhimu kwenye mradi huu.


       Wakili Gidion Kaino Mandesi, Mkurugenzi Mtendaji wa DOLASED amesema zipo sheria mbalimbali za nchi ya Tanzania na za kimataifa ambazo zinashughulikia masuala ya haki za ajira na kufanya kazi pamoja na kuwaendeleza na kuwalinda vijana wenye ulemavu. Mathalani, ibara za 22 na 24 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (kama ilivyorekebishwa); vifungu vya 30 – 34 vya Sheria ya Watu wenye Ulemavu na.9 ya mwaka 2010 pampoja na kanuni zake za mwaka 2012; Ibara ya 27 ya mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, 2006; Sheria ya Ajira na mahusiano kazini na.6 ya mwaka 2004 pamoja na Sheria za Kazi za Shirika la kazi Duniani (ILO Conventions).


      Sheria zote hizi zimeweka mazingira wezeshi na kutoa fursa za ajira kwa vijana wenye ulemavu kushiriki kikamilifu na kwa usawa kwenye sekta ya ajira na kazi. Kwahiyo, vijana wenye ulemavu wana haki ya kufanya kazi na kupata ajira za staha kwenye soko la ajira hapa nchini Tanzania kama ilivyo kwa vijana wenzao wasiokuwa na ulemavu, ili waweze kuishi kwa kufanya kazi na kujitegemea kwenye jamii. Kwa hakika, wana uwezo mkubwa, vipaji na nguvu kazi ya kutosha ya kuwawezesha kuishi kwa kufanya kazi ama kwa kuajiriwa na kuwezeshwa kujiajiri wenyewe kwa lengo la kujipatia kipato stahiki, haiba na heshima ndani ya jamii yetu.


 

2. MALENGO MAHSUSI

      Kuwezesha jamii kutambua kuwa, kila kijana mwenye ulemavu amapewa fursa sawa ya kupata haki ya ajira na kufanya kazi za staha kwa kuzingatia utu na sheria zilizopo. Pia, azma ni kuwawezesha vijana wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa zilizopo za kufanya kazi kikamilifu na kwa tija kubwa. Kuwahimiza waajiri kwenye sekta za umma na binafsi kutoa ajira kwa vijana wenye ulemavu bila ya ubaguzi kwa msingi wa ulemavu au aina yoyote ile.

 

3. CHANGAMOTO ZILIZOPO

     Nguvu kazi (Labour Force) ya vijana wengi wenye ulemavu bado halijatumika ipasavyo. Waajiri wengi hapa Tanzania bado hawajatimiza wajibu wao kisheria wa kutoa ajira kwa vijana wenye ulemavu. Wanaachwa nje ya soko la ajira.

     Mtazamo hasi kwenye jamii juu ya dhana ya ulemavu na vijana wenye ulemavu ni chngamoto kubwa na hivyo inakwamisha vijana wenye ulemavu katika suala la kupata ajira na kufanya kazi pamoja na kukopeshwa mikopo yenye riba nafuu kutoka taasisi za fedha na mikopo. Wanatengwa na kubaguliwa kwa mila na desturi potofu iliyopo ndani ya jamii zetu za Kitanzania kwa kuwaona kuwa hawajiwezi n ani watu wakupata msaada tu.


      Vikwazo vya ufikikaji kwenye taasisi na kwenye mazingira ya kufanyia kazi mahali pa kazi vinawazuia vijana wengi wenye ulemavu kupata fursa ya kuajiriwa n ahata kujiajiri wenyewe. Taarifa na matangazo ya nafasi za kazi kwenye soko la ajira hazipo  kwenye muundo unaofikika kwao; na kwahiyo, haziwafikii kwa wakati uliowekwa kuwasilisha maombi ya kazi. Wengi wanaachwa nyuma.


      Unyanyapaaji, kutengwa, kubaguliwa, kupuuzwa utekelezaji wa sheria za ajira na kazi kwa watu wenye ulemavu, kutofikika kwa miundombinu sehemu za kazi na ukosefu wa taarifa muhimu za ajira na kazi ni vikwazo vinavyozuia vijana wenye ulemavu kupata ajira na fursa za kufanya kazi nchini Tanzania.

 


 

4. MAZINGATIO MUHIMU KUHUSU MASUALA YA AJIRA NA KAZI

      Kufanya ushawishi na utetezi kwa umma wa Tanzania kuhusiana na kuwa na mtazamo chanya wa kuajiri vijana wenye ulemavu katika sekta ya ajira za umma na kwenye sekta binafsi. Aidha, kuwajulisha wananchi kuwa, Sheria mahsusi ya Watu wenye Ulemavu na.9, 2010 pamoja na kanuni zake za mwaka 2012 zimeweka masharti ya kisheria kwenye kifungu cha 31(2) kwenye sheria na kanuni ya 40(1) kuwa, asilimia tatu (3%) ya idadi ya wafanyakazi walioajiriwa na kila muajiri ni lazima wawe ni wenye ulemavu.


     Waajiri wote kwenye sekta ya umma na binafsi wahamasishwe na kuhimizwa na wananchi kuwa ni wajibu wao kisheria kutimiza masharti ya kutoa ajira kwa vijana wenye ulemavu na kuhakikisha wanatii kwa dhati sheria husika.

      Kuhakikisha wanaajiriwa wenye ulemavu wanafanya kazi kwa bidii na nidhamu kubwa, wanajua haki zao na wanadai kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu na.9, 2010 kupewa na waajiri wao msaada stahiki (reasonable accommodation) kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na tija kubwa.


      Aidha, mikataba ya ajira ya watu wenye ulemavu wanaoajiriwa na wale wafanyakazi waliopata ulemavu wakiwa kazini ajira zao zinalindwa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu na.9, 2010. Hawapaswi kuondolewa kazini kwa msingi wa ulemavu wao.

       Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na jamii kwa ujumla, inapaswa kusimamia na kuwezesha vijana wenye ulemavu wanapata fursa za kuajiriwa na kujiajiri wenyewe kwa ajili ya kufanya kazi na kujipatia kipato.


Kanuni ya malipo sawa kwa kazi sawa haipaswi kutumiwa vibaya na waajiri kuwanjima vijana wenye ulemavu haki ya kufanya kazi na kulipwa malipo stahiki. Waajiri wote wote wanapaswa kuzingatia kwa dhati masharti kwa mujibu wa ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

      Wananchi na wadau wote katika sekta ya ajira wana wajibu wa kuwawezesha vijana wenye ulemavu kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jitihada za kufanya kazi kwa nia za kuwasaidia kupata kipato na kazi kwa manufaa yao binafsi na taifa letu kwa ujumla.


      Serikali pamoja na taasisi za fedha na mikopo zina wajibu wa kuwasaidia vijana wenye ulemavu kupata fursa za mikopo zenye riba nafuu au ruzuku kwa ajili ya kuendeleza shughuli za biashara na uzalishaji ili kuwaongezea kazi za kipato vijana na watu wazima wenye ulemavu nchini Tanzania vijijini na mijini.

     Mikakati yote ya kuwainua vijana wenye ulemavu kiuchumi kwa kuwataftia fursa za ajira na kazi pamoja na mafunzo ya stadi za kazi itasaidia sana kupanua fursa za ajira kwao na kuhimiza waajiri kuwaajiri bila ya ubaguzi. Wanajamii wanatakiwa kuwaunga mkono kwa hali na mali vijana wenye ulemavu ili waweze kuishi kwa kufanya kazi zenye staha, ubora, zinazozingatia haki, mahitaji na utu wao.

Kupitia jitihada hizi, vijana wenye ulemavu wanapaswa kulindwa dhidi ya ukosefu wa kazi, unyonywaji na kufanyishwa kazi za shuluti. Pia, wanalindwa dhidi ya ubaguzi kwenye nyanja za ajira na kazi.


5. HITIMISHO

       Jamii ya Tanzania ina mchango na jukumu kubwa sana la kuwa na mtazamo chanya kuhusu vijana wenye ulemavu na haki zao za kupata ajira na kufanya kazi bila ya vikwazo vyovyote. Kwahiyo, serikali pamoja na jamii itasaidia kuongeza fursa za ajira na kazi, mafunzo yastadi za kazi, michakato ya kuajiri iwe wazi ana iwafikie kwa wakati vijana wenye ulemavu, miundo rafiki kwao kimawasiliano; kuajiriwa na kuendelezwa kazini, kuwawekea mazingira salama na mazuri kwenye sehemu za kazi na kutambua na kuheshimu haki, mahitaji na utu wao ni mambo muhimu ya kuzingatiwa.


     Vile vile, vijana wenye ulemavu kote vijijini na mijini nchini Tanzania, wana jukumu la kuzijua haki zao, fursa na wazichangamkie fursa za kiuchumi na ajira ili wazipate na kuzitumia kwa manufaa yao wenyewe na taifa letu kwa ujumla.

Vikwazo vyote ambavyo vinazuia fursa za ajira na kazi kwa vijana wenye ulemavu ni lazima viondolewe.

      Mtazamo chanya kwenye jamii kuhusiana na vijana wenye ulemavu na haki zao za kufanya kazi wanapaswa kuendelea kuimarishwa na kulindwa. Kuwa na programu za maendeleo na ujumuishwaji kwenye jamii kwa watu wenye ulemavu ni chachu na muelekeo sahihi kwa ustawi, mahitaji na haki zao kuzifurahia na kuzipata. Kuondoa vikwazo kwenye soko la Ajira ambavyo kwa kiwango kikubwa zinakwamisha vijana wenye ulemavu kuajiriwa na kujiajiri ni sharti vikaondolewa mara moja.

     Kuzingatiwa kwa sheria na kuwepo kwa mtazamo chanya wa jamii zitachangia sana kufungua fursa za ajira na haki kwa vijana wenye ulemavu. Hivyo basi, nguvu kazi ya vijana wenye ulemavu itaweza kutumika vizuri kwenye soko la ajira nchini Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post