Na John Mapepele
Wakaazi wa Hifadhi ya Ngorongoro ambao ni kaya 11 na wananchi 43 pamoja na mifugo 36 walioamua kuhama kwa hiari kupisha uhifadhi leo tarehe 19 Oktoba, 2023 wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Serikali kuanzisha zoezi hilo linalokwenda kuboresha maisha yao na vizazi vyao.
Wakaazi hao wanakwenda kuhamia katika maeneo waliyoyachagua wenyewe kwa hiari katika Wilaya za Monduli, Meatu, Arusha vijijini, Simanjiro na Handeni.
Akiongea mara baada ya kuagwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Raymond Mwangala ambaye alikuja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na mbele ya Kamishna Mteule wa Hifadhi ya Ngorongoro Richard Kiiza, Bi. Magdalena Isaya amemsifu Rais Samia kwa upendo mkubwa wa kuwaandalia huduma bora za jamii na kuwapa makazi bora huku akiwapatia chakula na kusisitiza kwamba maisha yao yalikuwa zaidi ya wanyama wa porini
“Mtoto wa Nyani ambaye anaishi porini hana utapiamlo lakini mtoto wangu ninayeishi naye porini/Hifadhini ana utapiamlo! Namshukuru sana Mama Samia kwa kuokoa maisha yetu” amefafanua Magdalena.
Aidha amepongeza hatua ya Serikali ya kuwafanya wakazi kuchagua kwa hiari maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
“Napenda kumshukuru sana Rais wangu kwa kuwa ametufungulia maisha mapya ya kupata maisha bora maana tulikuwa tunaishi maisha magumu yasiyokuwa na huduma bora za kijamii ndani ya hifadhi lakini sasa tunamshukuru ametuandalia kila huduma ya kijamii na sisi tunajisikia binadamu maana tunapata zaidi ya haki za kibinadamu “. Amefafanua Bi. Magdalena
Kwa upande wake Bwana Michael Kipuyo amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwaboreshea maisha yao huku akisisitiza kuwa ilikuwa vigumu kufanya maendeleo yoyote wakatiu wakiishi kwenye hifadhi kwa kuwa walikuwa hawaruhusiwi kufanya kazi zozote ikiwa ni pamoja na kufanya ujenzi na kilimo.
“Ninamshukuru Rais kule aikikuwa ngumu kufanya maendeleo maana ilikuwa huwezi kulima, kujenga na wala huwezi kumrithisha mtoto wako shughuli za maendeleo”. Ameongeza Kipuyo
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Mwangala amefafanua kuwa zoezi hili linafanyika kwa kufuata sheria zote za nchi, utu, na haki za binaadamu, tumepanua wigo zaidi ambapo pamoja na maeneo yaliyotengwa na Serikali mwananchi ana haki ya kuchagua popote anapotaka kwenda na Serikali itampa staki zake kwa mujibu wa sheria.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa kuhamisha watu awamu ya Pili Kamishna Msaidizi mwandamizi Mdala Fedes amebainisha kuwa Serikali imeongeza idadi ya nyumba zinazojengwa kutoka 503 za awamu ya kwanza hadi kufikia nyumba 5,000 katika awamu ya pili na kuongeza idadi ya huduma za kijimii kama vile maji, shule, vituo vya afya, umeme, barabara, mawasiliano na huduma za mifugo na posta.
Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa Nyumba umepanuka katika maeneo mengine ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Kilindi na Handeni ambapo nyumba 1500 zinatarajiwa kujengwa katika kijiji cha Kitwai B kilichoko Wilaya ya Simanjiro, nyumba 1,000 kijiji cha Saunyi kilichopo Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga na nyumba zingine 2500 zitajengwa katika kijiji cha Msomera kilichoko Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga.