23 Oktoba 2023, Arusha
Waajiri nchini wametakiwa kufuata na kuzingatia miongozo yote ya ajira ya kitaifa na kimataifa inayowaelekeza ikiwemo kuwapa wafanyakazi uhuru wao wa kujiunga na vyama wa wafanyakazi pasipo kuwaingilia katika maamuzi yao.
Wito huo umetolewa na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini Ndg. Donald Alacka, aliyemwakilisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista J. Mhagama (MB) katika ufunguzi wa Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE iliyoanza leo jijini Arusha ambapo sambamba na wito huo pia amewataka Wafanyakazi nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia taratibu na matakwa ya kazi zeo ikiwemo maadili ya Utumshi ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara ambayo i⁹naweza kuchangia kushuka kwa uzalishaji katika sehemu za Kazi.
Awali akiwasilisha risala kwa Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa TUGHE, Cde. Hery Mkunda, alibainisha kuwa Mafunzo haya yamekuwa yakiandaliwa na TUGHE kila mwaka kuanzia 2018 ambapo huwaleta pamoja Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE ili kujenga uelewa wa pamoja na kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa kuwa na utofauti wa uelewa juu ya taratibu mbalimbali za kiutumishi kaziniìì.
Pia Cde. Mkunda amebainisha kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini, bado zipo changamoto ambazo ameiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi kama vile kufanya maboresho ya viwango vya posho za kuitwa kazini kwa wafanyakazi wa kada za afya, kutolipwa malipo ya fedha za likizo ya kila mwaka kwa muda mrefu kwa watumishi wa Umma wasio walimu katika baadhi ya Halmashauri za Wilaya, kutolipwa stahiki za fedha za kujikimu kwa watumishi wapya, malimbikizo ya Madeni ya Mishahara kwa watumishi wa kada ya Afya baada ya zoezi la uhakiki kwa hosptali za CDH za Nyakahanga, Bihalamulo, Murugwanza na Nyakahanga. Pia alibainisha changamoto ya baadhi Waajiri kuingilia uhuru wa Watumishi kujiunga na Chama cha wafanyakazi kwa hiari yao kwa kuwachagulia Chama cha Kujiunga hata kama Chama hicho sio Sekta yake husika pamoja na changamoto ambazo zinawakabili Watumishi wenye mahitaji maalum.
Semina hii imehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Joel Kaminyoge, Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Dkt Jane Masunzu Madete, Wajumbe wa KUBK, Viongozi wa Serikali na Wakuu wa Taasisi mbalimbali pamoja na viongozi wa TUGHE kutoka ngazi ya Taifa hadi tawi ambapo itaendeshwa kwa takribani siku tano (5) huku mada mbalimbali zikifundishwa.
Pia semina hii itaenda sambamba na washiriki wote kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea mbuga ya Wanyama ya Tarangire.
Imetolewa na Idara ya Habari na Uhusano
TUGHE