UTAFITI WA VIASHIRIA, MATOKEO YA VVU NA UKIMWI UMEKAMILIKA HUKU KUKIWA NA MATOKEO CHANYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na  Uratibu Jenista Mhagama  wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kukamilika kwa utafiti viashiria na Matokeo ya VVU na Ukimwi Nchini Tanzania kwa Mwaka 2022/2023 


Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog, Dodoma. 

Taarifa za Utafiti wa viashiria na Matokeo ya VVU na Ukimwi Nchini Tanzania kwa Mwaka 2022/2023 zimekamilika huku takwimu za Utafiti huo zikitarajiwa kutolewa rasmi Desemba Mosi Mwaka huu Mkoani Morogoro katika Maashimisho ya siku ya UKimwi Duniani.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 31,2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na  Uratibu Jenista Mhagama  wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kukamilika kwa utafiti huo na kueleza kuwa Utafiti huo unaonesha Tanzania imepata matokeo chanya kutokana na idadi ya Maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kuendelea kupungua ikilinganishwa na Utafiti uliofanywa  2016/2017.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ni mafanikio mazuri ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafikia kuelekea kufikia Malengo ya kitaifa ya kufikia SIFURI TATU – yaani Kutokuwa na Maambukizi Mapya, kutokuwa na unyanyapaa na ubaguzi, na Kutokuwa na Vifo Vitokanavyo na UKIMWI. 

Waziri Mhagama ameeleza lengo la utafiti huo kuwa ni kupima mwenendo wa maambukizi mapya  ya Virusi vya Ukimwi Nchini ikiwa ni pamoja na kuisaidia nchi kuchukua hatua katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi  na Ukimwi na kujitathimi. 

"Lengo la utafiti huu ni kupima matokeo ya juhudi za mapambano dhidi ya UKIMWI, kupitia utafiti huu, tutapata taarifa kuhusu viashiria na matokeo ya VVU/UKIMWI katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2022/23 ambazo ni takwimu muhimu kuhusu hali ya UKIMWI nchini, "amefafanua Waziri huyo

Amefafanua kuwa utafiti huo uliokamilika ni utafiti wa tano ambapo nchi hufanya tafiti kila baada ya Miaka mitano ili kujipima katika mapambano dhidi ya Ukimwi ambapo umeshirikisha Wataalam mbalimbali wa Tanzania Bara ,Zanzibar na Wataalam toka nje ya Nchi.

"Kwa taratibu zilizopo huwa tunaanza kutoa taarifa kisha baada  ya muda tunatoa matokeo,kwa Serikali yetu huu utafiti si wa kwanza imekuwa ikifanya utafiti kila baada ya miaka Kitano na utafiti wa mwisho ulifanyika 2016/2017 lengo kujaribu kupima matokeo ya juhudi zero ndani ya taifa na kupambana  dhidi ya ukimwi, "amesema

Pamoja na hayo ameeleza kuwa,"Utafiti huu umefanywa  na Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ,Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu,Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar  kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Serikali zikiwemo Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa - CDC ,Kituo cha Kudhibiti Magonjwa na Kinga na Chuo Kikuu cha Columbia, "amesema

Amewataja Wadau wengine ni Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango Jumuishi wa kupambana na UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma  na kufafanua kuwa Kazi hiyo  imefanyika kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI - PEPFAR. 

"Natoa  wito kwa wananchi kupokea taarifa hii ya awali na kujiandaa kupokea matokeo rasmi ya utafiti huu ifikapo Disemba Mosi, 2023, " Amesema.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post