TBS YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUTHIBITISHA UBORA BIDHAA ZAO


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara nchini kuthibitishwa ubora wa bidhaa zao hatua itakayowawezesha kukua kibiashara pamoja na kuamika kwa watumiaji wa bidhaa husika.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Uthibiti Ubora wa TBS, Pius Mwakalinga, wakati akizungumza na washiriki wa Maonesho ya Biashara yaliyoandaliwa na Chemba ya Biashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) yaliyofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 mwezi Oktoba kwenye Uwanja wa Stendi ya Zamani Mjini Babati mkoani Manyara.

Alisema ili kukuza biashara ni muhimu wazalishaji wakathibitisha ubora wa bidhaa zao TBS, ambapo huduma hiyo inatolewa bure kwa wajasiriamali, kwani gharama zao zinalipwa na Serikali.

Alisema ili wajasiriamali wathibitishiwe bidhaa zao wanatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka SIDO na baada ya hapo, TBS inaanza mara moja mchakato wa kuthibitisha biashara zao bure.

"Wajasiriamali wanatakiwa kupitia SIDO na baada ya kupewa mafunzo watapewa barua ya utambulisho wakiileta kwetu, maofisa wetu watafanya ukaguzi kwenye maeneo yao ya uzalishaji na kuchukua sampuri za bidhaa wanazozalisha na kuzipima kwenye maabara ili kujiridhisha kama zinakidhi ubora," alisema Mwakalinga na kuongeza;

“Serikali kupitia TBS tunatoa huduma kwa wajasiriamali kwa miaka mitatu, lakini pia tunawashauri wapitie SIDO, kule wanapewa mafunzo hivyo anavyokuja kwetu na barua ya SIDO itamwezesha kumtambulisha huyo mjasiriamali.”

Mwakalinga alisema kuanzia mwaka wa nne mjasiriamali ataanza kulipia robo ya gharama za upimaji na uthibitishaji ubora bidhaa anazozalisha.

Kwa mujibu wa Mwakalinga, hatua hiyo inalenga kumwezesha kukua kibiashara na baada ya hapo ataanza kulipia gharama zote upimaji na uthibitishaji bidhaa mwenyewe kwa maana wanaamini atakuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na shirika hili kuhakikisha soko la Tanzania linakuwa na bidhaa zilizothibitishwa ubora, Mwakalinga alisema wanaendelea hufanya ukaguzi wa kushutukiza kwenye soko na sehemu za uzalishaji kwa kushtukiza na kuchukua sampuri, ambazo hupimwa kwenye maabara za shirika ili kujiridhisha kama wazalishaji wanaendelea kuzalisha bidhaa kwa kukithi matakwa ya ubora.

Alisema wanafanya hivyo kwa sababu baadhi baadhi ya wafanyabishara sio waaminifu, ambapo hufanya uchakachuaji wa bidhaa.

Aliwataka wazalishaji wenye tabia hiyo kuacha mara moja, kwani wakibainika bidhaa zao zitaondolewa sokoni, kuteketezwa kwa gharama zao na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alifafanua kwamba uthibiti ubora wa bidhaa ni kwa mujibu wa sheria ya viwango namba mbili ya mwaka 2009 inayoweka masharti ya uimarishaji wa viwango vya vipimo vya bidhaa na huduma.

Kwa mujibu wa Mwakalinga miongoni mwa majukumu ya Shirika ni kukuza viwango, usalama na uhakikisho wa ubora katika tasnia na biashara na kupitia ukuzaji wa viwango, uthibitishaji, usajili, ukaguzi, upimaji na huduma za vipimo kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post