TARURA YAWAUNGANISHA WANANCHI WILAYA YA RUANGWA NA LIWALE



Na Catherine Sungura, Lindi. 

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Lindi imekamilisha ujenzi wa daraja la Mbwemkuru lenye urefu wa mita 75 na kufungua barabara ya Ruangwa-Nangurugai- Kiangara-Mirui-Mbwemkuru yenye jumla ya Km 65.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Narubi ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja  hilo imekua ni fursa kwa wananchi kusafiri kwa urahisi kutoka Ruangwa kwenda Liwale.

"Daraja hili ni muhimu kwa wananchi wa wilaya zote mbili katika kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao, tumejenga daraja na kufungua barabara na sasa magari yanapita hapa kwenda Liwale ", amesema mhandisi Narubi.

Naye, Bi. Sharifa Majaliwa mkazi wa Kijiji cha Nangurugai amesema kuwa kabla ya kujengwa Daraja hilo ilikuwa vigumu kwao kufanya shughuli za kilimo ng'ambo ya pili ya mto lakini kwa sasa wanavuka na kufanya kazi zao kwa urahisi.

"Kutoka hapa Nangurugai kwenda Mirui ilikua ni vigumu, mto una mamba na tulikua tukivuka kwa kutumia njia hatarishi lakini sasa tunashukuru Serikali kwa kukamilisha daraja hili,  amesema Bi Sharifa.

Kwaupande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mirui, Bw.  Chande  Ally amesema kuwa mwanzoni Kijiji hicho kilikuwa hakifikiki kwani mtu alikuwa hawezi kutoka Mirui kwenda Ruangwa kwa urahisi.

"Kijiji chetu kilikua Kisiwani, ufunguzi wa barabara hii na kukamilika kwa daraja la Mbwemkuru limefungua fursa kubwa za kiuchumi na kijamii", amesema Bw. Chande.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kufungua barabara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha wanachi kufika kusikofikika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post