SHEIKH MSAFIRI KITUMBO AMFANANISHA MASELE NA NGAMIA, ATAJA SIFA KUU TANOSheikh maarufu Manispaa ya Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla Sheikh Msafiri Kitumbo ambaye pia ndiye Mratibu wa Maulid za Mtume Mohamed S.A.W Kanda ya ziwa amempongeza na kumfananisha Mhe. Stephen Masele ambaye ni Mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika mstaafu na mnyama aliyetakaswa Ngamia kwa sifa zake.

 Akizungumza wakati wa Maulid, baada ya Masele kutoa ngamia, Sheikh Kitumbo alizitaja sifa kuu tano za ngamia na kuzifananisha na sifa na tabia ya mhe Masele kama ifuatavyo:-


1. UPENDO- Ngamia katika kitabu cha Quran takatifu kuna aya inayomzungumzia upendo wa ngamia, ni kiumbe kilichotakaswa, Mtume Mohamed S.AW alitumia sadaka ya ngamia kueneza upendo, amani na uvumilivu kwa Waislamu na watu wote duniani. Masele ana upendo kama wa ngamia , ana upendo wa dhati kwa watu bila kuwabagua kwa hali zao za kimaisha, ni mtu wa watu, watu wanampenda kwa dhati ndani ya mioyo yao. Masele ni mtu aliyejaa kwenye mioyo ya watu.


2. UVUMILIVU- Ngamia ni mnyama mvumilivu sana, anaweza kuishi katika hali yoyote ya mateso jangwani bila maji kwa muda mrefu na akavumilia, Masele ni mvumilivu sana , amepitia mambo magumu sana lakini ameonesha kiwango kikubwa cha uvumilivu na ukomavu.


3. FURAHA- Ngamia ni mnyama anayeleta furaha kwa watu, kama ilivyo kwa Masele ni mtu wa watu anayependa furaha na kuleta amani na upendo kwa watu wote bila kujali hali zao za kimaisha.


4. UKUBWA: Ngamia ni kiumbe kikubwa- Kumvaa ngamia lazima ujipange, kumvaa Masele lazima mtu ajipange, Masele ni mwanasiasa mkubwa wa kitaifa na kimataifa .


5. UPOLE:- Ngamia ni mnyama mpole sana, ana huruma sana anatembea kwa malingo, anajiamini, hababaishwi na mazingira yoyote. Ndivyo ilivyo kwa Masele ni mtu mpole sana, ana huruma sana, anasaidia sana watu wenye shida mbalimbali iwe ni misiba, harusi, makanisani, misikitini na hata kusaidia wanafunzi wanasoma. Ukiwa na shida ukipeleka kwa masele utapata tu msaada uwe wa mawazo ama pesa. Masele ana moyo wa utajiri wa roho, sio mchoyo ni mtu wa kujitoa kwa watu katika hali na Mali, katika shida na raha.

Naye Sheikh wa mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke  amemmwagia sifa nyingi Mhe Masele kwa kusema kuwa hana deni kwa Waislamu, amefanya kitu adimu na kinachoheshimika sana katika dini ya uislamu.

“Kitendo cha mhe masele kutoa sadaka ya Ngamia katika Maulid ya Mtume Mohamed S.AW kimeheshimisha sana uislamu, hakika Masele hana deni kwetu sisi waislamu, tutamuombea duwah Kila siku na Mwenyezi amtimizie haja zake”, aliongeza sheikh Kabeke ambaye ni sheikh wa mkoa wa Mwanza.


Naye sheikh wa mkoa wa Shinyanga Ismail Habib Makusanya alimfananisha Mhe Masele na Mfalme wa Ethiopia aliyekuwa mkristo lakini akajitolea kumpatia “Mahali” ya kuolea Mtume Mohamed S.A.W ili afunge ndoa. 

Aliongeza Sheikh Ismail kuwa “Tangu nilipomfahamu mhe Masele miaka zaidi ya 20 iliyopita hajabadilika kitabia awe na cheo ama asiwe na cheo masele ni yule yule mtu wa watu, kijana mwenye heshima, upole, upendo na ni mtu wa msaada. Amekuwa akisaidia jamii Kila kukicha iwe wagonjwa, iwe misiba, iwe harusi, iwe ada za wanafunzi wewe kama una jambo lako mpelekee masele utapata ufumbuzi. Ni kijana mwema sana”.


Viongozi wa kidini walioudhuria Maulid hiyo walimiminia sifa nyingi kwa jinsi wanamfahamu mhe Masele wakiwemo masheikh mkoa wa Simiyu sheikh Kwezi, na wengine wengi. Sheikh Kwezi alisema “Mhe Masele amefanya jambo kubwa sana katika uislamu, ameandika historia kubwa katika mioyo ya Waislamu kwa kufanya jambo alilolipenda Mtume wetu S.A.W, na sisi waislamu tutakuunga mkono katika jambo lako lolote utakalo hitaji msaada wetu”

Mgeni rasmi katika Maulidi hiyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Taifa(BAKWATA) Sheikh NUR Mruma amemwagia sifa mhe Masele na kusema ni watu wachache sana wenye moyo wa kujitoa kwa ajili ya wengine kama masele alivyoonesha.

"Tangu nifike shinyanga nimesikia sifa nyingi nzuri za masele kwa jamii, kwamba ni mtu wa msaada sana” endelea na moyo huo na Mwenyezi Mungu atakulipia, atakulipa wema wako kwa jamii yako. Natoa maelekezo na wito kwa masheikh wote wa shinyanga na Kanda ya ziwa kumuombea duwah Masele kila manapokuwa na shughuli zenu ili Mwenyezi Mungu azidi kumlinda dhidi ya mabaya yote, ampe ulinzi na kujalia siha njema” aliongeza sheikh Mruma.


Mh Stephen Masele amewahi kuwa mbunge wa Shinyanga Mjini, Naibu Waziri katika wizara mbali mbali katika serikali ya Rais Kikwete na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika chombo cha Umoja wa Afrika chenye makao makuu nchini Afrika Kusini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post