DKT. BITEKO AWATAKA TANESCO, REA KUFIKISHA UMEME KWENYE VITONGOJI

*Awasha umeme Mtanana Kongwa

*Sasa kijijini kama mjini

Na Mwandishi Maalumu,Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wananchi waliopo kwenye vitongoji wanapatiwa umeme ili kuharakisha maendeleo yao kiuchumi.

Mhe. Dkt. Biteko ameyasema hayo alipokuwa akiwasha umeme kwenye Kijiji cha Ndalibo, Kata ya Mtanana Wilaya ya Kongwa sambamba na kuzindua kisima cha maji ambacho kitakuwa kikitumia umeme kwa manufaa ya wananchi wa eneo hilo.

"Ndugu zangu niwahakikishie, Rais Dkt. Samia anapambana usiku na mchana kuhakikisha umeme unapatikana na kuinua hali za maisha ya wananchi waliopo vijijini kwani umeme sio anasa bali ni jambo la muhimu kwa sasa," amesema Dkt. Biteko.

Aidha, amewaagiza TANESCO na REA kuhakikisha Vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme kuhakikisha vinawekewa huduma hiyo muhimu kwa haraka. 

Awali akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule aliishukuru TANESCO na REA kwa kazi kubwa inayofanywa katika mkoa huo ya kuhakikisha umeme unapatikana pamoja na usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya wilaya hiyo zinazotolewa na Mhe. Rais Samia. 

Alisema mahitaji ya umeme kwa Mkoa wa Dodoma ni makubwa na kumekuwa na ongezeko la viwanda na shughuli za kiuchumi hivyo ni vema taasisi hizi zikafanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo kwa wanachi

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mhe. Job Ndugai ameikumbusha  REA kupeleka umeme kwa wakati katika maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa na nishati hiyo hususan vitongoji vya Chinangali, Chamwino na Manzese na kuwataka TANESCO na REA kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma hiyo ya umeme. 

"Tunashukuru sana jitihada za Mhe. Rais Samia kutenga fedha kwa ajili ya masuala ya nishati, hii imekuwa na msaada mkubwa kwa wananchi wa Kongwa hususan katika kuleta maendeleo ya wananchi wetu," alisema Mhe. Ndugai.

Mradi huo wa maji uliasisiwa na Mwalimu Abdi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Mtanana na tayari visima 25 vimeshawekewa umeme ili wananchi wapate huduma bora katika wilaya hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post