MAKONDA ATINGA NA BODABODA OFISI ZA CCM DAR, MAPOKEZI YAKE YAWEKA REKODI


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

PAUL Makonda amepokelwa kwa staili ya aina yake baada ya kutumia usafiri bodaboda wakati akienda Ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi(CCM)zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar ea Salaam ambako yamefanyika mapokezi makubwa.

Mapokezi ya Makonda yamefanyika leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tu Chama Cha Mapinduzi( CCM) kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho na leo amepokelewa rasmi na wana CCM mkoa wa Dar es Salaam .

Akitumia usafiri wa bodaboda akiendesha mwenyewe alifika Ofisi za CCM saa nne asubuhi akiwa na waendesha bodaboda kadhaa na baada ya kuwasili aliingia ofisini na kisha kuzungumza na waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Idara ya Itikadi na Uenezi.

Pia yamefanyika makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi Sophia Mjema ambaye ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais katika masuala ya wanawake na makundi maalum.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi na vitendea kazi, Makonda amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa kumpa kibali cha kuwatumikia watanzania katika bafasi hiyo lakini pia anamshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na Kamati Kuu kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kukitumikia Chama hicho.

"Namuomba Mungu anipe hekima, busara , uadilifu na maarifa ili kuifanya kazi hii kwa uaminifu na ukamilifu wa hali ya juu ili nisimuabishe Mungu na nisimuabishe Mwenyekiti wa Chama aliyeriki jina lake kwenda Kamati Kuu."

Pamoja na hayo Makonda ametumia nafasi hiyo kuwaomba watumishi na watendaji wa Chama hicho kumpa ushirikiano na kubwa zaidi kumpa taarifa sahihi ambazo zitamuwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri.

"Duniani kote watu wanaishi kwa taarifa na taarifa ndio inafanya maamuzi ,ukiwa na chanzo kibovu utafanya maamuzi mabovu na ukiwa na chanzo kizuri utafanya maamuzi sahihi, " amesema Makonda

Hivyo amesema anatarajia atapewa taarifa sahihi ili aweze kufanya ya kumsaidia Katibu Mkuu wa Chama ,kumsaidia Makamu Mwenyekiti,kumsaidia Mwenyekiti wao wa Chama na hatimaye kwa pamoja waweze kukiimarisha na kukijenga Chama kwa wananchi.

Makonda akitumia nafasi hiyo amewashukuru waandishi wa vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kushirikiana na CCM na kwamba waandishi wa habari wamekuwa kiunganishi kikubwa kati ya Chama na wananchi , hivyo Chama hicho kitaendelea kushirikiana na vyombo vya habari.

Aidha Makonda amemtakia majukum mema aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Sophia Mjema na kwamba anaamini watashirikiana katika kuyasemea makundi mbalimbali

Makonda akizungumza na waandishi wa habari amehitimisha mazungomzo yake kwa kueleza kwa sasa anaendelea kujifunza kuhusu nafasi yake na atajifunza kupitia watangulizi wake kuanzia Sophia Mjema, Shaka Hamdu Shaka na Nape Nnauye.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post