WAAJIRI WATAKIWA KUSIMAMIA MAADILI YA UONGOZI

 Na  Dotto Kwilasa, Dodoma


WAZIRI wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala bora George Simbachawene amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanasimamia na kuimarisha uzingatiaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Watumishi wa Umma.

Aidha amezielekeza Mamlaka za nidhamu kuendelea kufuatilia na kuchukua kwa wakati hatua stahiki dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.

Waziri Simbachawene ameeleza hayo leo Sept 21,2023  kwenye ufunguzi wa kikao kazi kati ya Ofisi hiyo na Taasisi simamizi za maadili ya kitaaluma lengo likiwa ni kuendelea kujenga ushirikiano wa usimamizi wa Maadili katika Utumishi wa Umma na kubadilishana uzoefu na taarifa zinazojumuisha mafanikio na changamoto za usimamizi wa maadili katika Utumishi wa Umma.

Amesema kikao kazi hicho kinatathmini utekelezaji wa Maazimio na Mpango Kazi wa Kikao kilichopita ili kubaini mafanikio na changamoto zilivyopanwa katika utekelezaji wa maazimio hayo na kuja na mapendekezo ambayo yatasaidia Serikali kuimarisha uadilifu katika Utumishi wa Umma.

"Nahimiza matumizi ya Serikali Mtandao ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa Maadili katika Utumishi wa Umma natoa rai kwenu, kwamba mikakati hiyo iandaliwe kwa lengo la kukuza Uwajibikaji na Usikivu wa Umma kama moja ya msingi wa Utawala Bora,"amesema .  

Amesema wajibu wa kusimamia Maadili ya Watumishi wa Umma na Utawala Bora katika Utumishi wa Umma ni suala mtambuka hivyo wapaswa kuendelea kushirikiana na kuwekeza katika mikakati ambayo itachangia kukuza Uwajibikaji na Usikivu wa watoa huduma kwa wananchi hususani katika maeneo yanayoigusa jamii moja kwa moja au kulalamikiwa mara kwa mara. 

"Mnapaswa kuangalia maeneo ya pamosekta ya Afya, Elimu, Ujenzi, Ardhi, Manunuzi na Ugavi kwa kuweka mifumo ya uwajibikaji na kuzishirikisha Taasisi Simamizi za Maadili na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma katika ukuzaji na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma,"amesisitiza 

 Waziri huyo ameeleza kuwa matarajio hayo yatafikiwa iwapo kuna ushirikiano wa kuandaa, kuhuisha na kutoa Miongozo mbalimbali ya kusimamia Uadilifu katika Utumishi wa Umma, kujenga uelewa wa miongozo hiyo kwa umma na kufanya ufuatiliaji wa uzingatiaji wa Maadili kwa mujibu wa miongozo.

"Kama mnavyofahamu hivi karibuni ofisi yangu ilihuisha Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005 na Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Malalamiko ya Wananchi wa mwaka 2012,kufuatia kuhuishwa kwa miongozo hiyo, kwa sasa ofisi imetoa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2023 na Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Mrejesho wa Wananchi kuhusu Huduma Zinazotolewa na Serikalini,"amesema

Licha ya hayo amesema kuwa Taasisi Simamizi za Maadili na Utawala Bora pamoja na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma ni miongoni mwa Taasisi ambazo hupokea malalamiko mbalimbali kuhusu ukiukwaji wa Maadili ya Utumishi na ya Kitaaluma, hivyo Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Mrejesho wa Wananchi wa mwaka 2023 utasaidia kuimarisha utaratibu wa kushughulikia mrejesho kuhusu huduma zinazotolewa.

"Matarajio ni kuwa mtazingatia maelekezo yaliyomo katika miongozo hiyo,matarajio yangu kuwa mikakati itakayofikiwa katika kikao itasaidia kuondoa malalamiko kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili katika maeneo ambayo yanalalamikiwa katika Taasisi hizo kwa sababu wanasimamia upatikanaji wa haki,"amesisitiza Simbachawene 

Amesema ili kutokomeza malalamiko ambayo yanaelekezwa katika Taasisi za Umma,  Taasisi Simamizi za  Maadili na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma zinapaswa  kutoa elimu kwa wanataaluma ili wazingatie miiko ya taaluma zao, mafunzo ya Maadili kwa watumishi wa umma ili wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Maadili ya utendaji kazi na yale ya kitaaluma. 

"Lazima kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu ambapo Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma mnapaswa kusimamia na kuchukua hatua stahiki kwa wakati kwa wale wanaokiuka Maadili ya taaluma ,shughulikieni kwa wakati malalamiko yote,"amesema 

Kwa upande wa Taasisi Simamizi za Maadili na Utawala Bora Waziri huyo amesema,zinatakiwa kufuatilia uzingatiaji wa Maadili ya Viongozi na Watumishi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazowaongoza. 

"Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma kutoa ushauri wa kitaalamu, kutoa ushauri katika mapitio na maboresho ya Kanuni za Maadili ili kuleta mabadiliko,"amesema .
Mwisho Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post