NAIBU WAZIRI BYABATO AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA BIASHARA WA JAMAICA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Wakili Stephen Byabato(Mb) amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica Mhe. Kamina John Smith pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77+ China unaofanyika jijini Havana nchini Cuba.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea kuridhishwa kwao na hali ya uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Jamaica na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi ili kuimarisha uhusiano huo.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Byabato amemuelezea Mhe. Smith kuwa Tanzania inaridhishwa na uhusiano mzuri uliopo na kuongeza kuwa kuna haja ya kuhakikisha uhusiano huo wa kidplomasia unaimarishwa na kufikia hatua ya juu.

Amemhakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Jamaica katika maeneo yatakayozinufaisha pande zote mbili.

Pia amemuelezea nia ya Tanzania ya kupanua wigo wa maeneo ya ushirikiano na kuingiza sekta za uchumi wa bluu, biashara na uwekezaji.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica Mhe. Kamina John Smith alisema pamoja na uhusiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania, Jamaika inaiomba Tanzania kuiunga mkono katika nafasi mbili inazogombea kimataifa katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Bahari (IMO) na Kamati ya Urithi wa Dunia iliyoko chini ya UNESCO.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post