RITA: WOSIA UNAEPUSHA MIGOGORO KWENYE FAMILIA


Afisa Sheria kutokaWakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Grace Shao, akitoa huduma kwa wananchi waliofika kwenye banda la taasisi hiyo katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Bariadi Mkoani Simiyu, ambako inaendelea Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign)
Na Derick Milton, Simiyu.

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imewataka watanzania kujenga tabia ya kuandika wosia, kwani kufanya hivyo itasaidia kwa kiwango kikubwa kuepusha migogoro ya mara kwa mara kwenye familia na kuwawezesha warithi halali kupata haki yao kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa Habari Kwenye Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) inayoendelea Mkoani Simiyu, Afisa Sheria kutoka RITA Grace Shao ameitaka jamii kuacha woga kuandika Wosia, kwani kufanya hivyo siyo uchuro na kusema baadhi ya watu wameandika na wanaendelea kuishi vizuri huku waliondika na wakafariki familia zao zimeendelea kuishi bila ya migogoro.


“ Familia nyingi zimekuwa na migogoro ya mara kwa mara juu ya mirathi, wengine wamedhulumiwa na ndugu ambao kisheria siyo waridhi wa mali, tumeendelea kuwaelimisha wananchi kuwa mwarobaini wa haya ni Wosia,” amesema Shao.

Aidha Shao amewasihi wananchi kutumia taasisi ya RITA Katika kuandaa wosia kutokana na kuwa chombo cha serikali, lakini pia ni taasisi ambayo haina ukomo wa maisha pamoja na kuwa na wanasheria wabobevu wa masuala ya wosia na mirathi.

Katika hatua nyingine Shao amewahimiza wazazi kujenga tabia ya kuwatafutia vyeti vya kuzaliwa watoto ili kuondoa usumbufu wanaoweza kupata pindi watakapotakiwa kwenda kuanza shule na kuhitaji cheti cha kuzaliwa.

Amesema kuwa kwa sasa mtoto akitakiwa kwenda kuandikishwa shule lazima awe na cheti za kuzaliwa, kupata cheti cha kuzaliwa ni muhimu pia lakini pia ili mtu apate Bima ya Afya lazima cheti za kuzaliwa awe nacho.

“Tunawasihi wananchi mtoto akizaliwa ndani ya siku 90 ni muhimu kumtafutia cheti cha kuzaliwa, hii itasaidia kumtengenezea mtoto msingi mzuri wa majina yake pamoja na kumbukumbu yake ya tarehe za kuzaliwa”, amesema Shao.

“ Kuna changamoto kubwa ya watu majina yao kuwa na shida, utakuta jina la shule ni tofauti na jina kuzaliwa, ikiwa hivyo huyo mtoto atapata shida wakati wa kutafuta kazi, lakini cheti cha kuzaliwa kinapotafutwa mapema inasaidia mtu kuwa na mtiririko mzuri wa majina yake,” ameongeza Shao.

RITA inaendelea Kutoa Huduma ya Usajili na kutoa Vyeti vya vya kuzaliwa,Elimu ya Mirathi,Kuandika na Kuhifadhi Wosia kwenye Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea kwenye viwanja vya Stendi ya zamani Mkoani Simiyu
Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, wakiendelea kupata huduma mbalimbali kwenye banda la Wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (RITA), katika Kampeni ya msaada wa kisheria wa ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) inayoendelea katika viwanja vya stendi ya zamani Mjini Bariadi mkoani Simiyu.
Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, wakiendelea kupata huduma mbalimbali kwenye banda la Wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (RITA), katika Kampeni ya msaada wa kisheria wa ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) inayoendelea katika viwanja vya stendi ya zamani Mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post