MWENGE WA UHURU 2023 WAZINDUA MRADI WA MAJI KIJIJI CHA KISIMA CHA NDEGE ULIOTEKELEZWA NA WATER MISSION





Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Abdalla Shaib Kaim amezindua Mradi wa Maji kijiji cha Kisima cha Ndege Wilaya ya Bahi  uliogharimu kiasi cha shilingi 586,099,100/= na kuridhishwa na ujenzi huo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi  huo ambao umefadhiliwa na kutekelezwa na Shirika la Water Mission uliofanyika Septemba 29,2023 katika Kijiji cha Kisima cha Ndege, Kata ya Msisi tarafa ya Mundemu Kaim amewataka wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji  ili kuweza kujipatia kipato nakukuza uchumi wa taifa.


Akitoa Taarifa ya mradi huo Meneja wa Shirika la Water Mission Mkoa wa Dodoma Benety Malima  Kwa Niaba  Mkurugenzi Mkuu amesema  Mradi huu utawanufaisha wananchi wa Kijiji cha Kisima cha Ndege wapatao 5,564.

“Fedha zilizotolewa na Shirika la Water Mission. Katika fedha hizo kiasi cha shilingi 12,605,600 ni mchango wa wananchi waishio katika kijiji cha Kisima cha Ndege,” amesema.


“Faida za mradi ni Kuwawezesha wananchi wa kijiji cha Kisima cha Ndege kupata huduma ya maji safi na salama ya kutosha kwa matumizi ya kawaida na ya kiuchumi, kupunguza maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama na kuwapatia wananchi muda wa kutosha kufanya shughuli nyingine za kiuchumi", ameongeza Malima.


Aidha, amesema matarajio ya mradi huo ni kuwapatia wananchi huduma bora na endelevu pamoja na kupanua miundombinu ya maji na kuongeza vyanzo vipya kulingana na ongezeko la watu na mahitaji.


Mbali na hayo amesema  Jumla ya miti mia mbili thelalini (230) imepandwa kwenye eneo la matenki na chanzo kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kulinda chanzo cha maji.
Hivyo kazi zote tajwa zimetekelezwa na kukamilika kwa asilimia 100.


Mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 27 Aprili, 2023 na kukamilika tarehe 29 Julai, 2023 ni moja kati ya miradi 13 ambayo Shirika la Water mission limetekelza katika mkoa wa Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post