NHC YATAKIWA KUTILIA MKAZO UKUSANYAJI MADENI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa uwasilishaji taarifa ya shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 25 Agosti 2023.

****************

Na Munir Shemweta, WANMM

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linatilia mkazo ukusanyaji madeni ya wapangaji katika nyumba zake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Timetheo Mnzava amesema, pamoja na shirika hilo kujitahidi katika ukusanyaji malimbikizo ya kodi za wapangaji wake lakini bado linatakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni kutoka kwa wadaiwa.

Akizungumza wakati wa Kikao cha kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dodoma tarehe 25 Oktoba 2023, Mhe. Mnzava amelitaka pia shirika hilo kuweka msisitizo zaidi katika kuzuia kuzalisha madeni badala ya kusubiri mpaka wapangaji kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii wametaka kuwepo mikakati madhubuti itakayowaogopesha wapangaji ili waweze kulipa kodi zao kwa wakati

Vile vile, Kamati hiyo imeonesha kuridhishwa na utendaji kazi wa shirika hilo katika kutekeleza miradi yake ambapo wamelitaka Shirika kuangalia namna ya kujenga nyumba za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi.

‘’Niipongeze NHC pamoja na Wizara ya Ardhi maana kazi za shirika zinaonekana hata kwa macho ila nisisitize muweke jitihada pia katika ukarabati wa nyumba zenu ili wapangaji wakae vizuri’’ alisema mjumbe wa kamati Cecilia Paresso.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza mbele ya Kamati hiyo amesema, kwa sasa upo uhitaji mkubwa wa nyumba na serikali iko katika marekebisho ya sera ili kuwezesha ushiriki wa taasisi na sekta binafsi katika uzalishaji nyumba.

‘’Kama serikali tutahakikisha kasi ya ujenzi wa nyumba inaongezeka maana takwimu za sensa ya watu na makazi zimeonesha uhitaji mkubwa wa nyumba na uzalishaji ukiwa mdogo hivyo msisitizo ni kuzalisha nyumba za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi’’ alisema Dkt Mabula.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa katika kikao cha kupokea taarifa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 25 Agosti 2023 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Lucy Kabyemera akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa uwasilishaji taarifa ya shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 25 Agosti 2023.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava akizungumza wakati Kamati yake ikipokea taarifa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 25 Agosti 2023 jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah akiwasilisha taarifa ya Shirika lake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii jijini Dodoma tarehe 25 Agosti 2023.
Sehemu ya watendaji wa Wizara wa Wizara ya Ardhi pamoja na wale wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiwa katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kupokea taarifa ya NHC jijini Dodoma tarehe 25 Agosti 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post