NAIBU WAZIRI KATAMBI ASISITIZA WAAJIRI WOTE KUWASILISHA MICHANGO NA TOZO MBALIMBALI KWENYE MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII, WCF, PSSSF NA NSSF

 


NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (wapili kushoto) akimpongeza Mwajiri ambaye ni Mwanachama wa WCF, Bw. Isani Longo kutoka kampuni ya Elfatel Enterprises Company Limited iliyoko Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambaye alifika kwenye banda la WCF kupata elimu ya fidia kwa wafanyakazi. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma ( wapili kulia) na  Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Zanzibar (ZEA) Bw.  Juma Buruhani Mohammed 

 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amewataka waajiri kote nchini kuhakikisha wanalipa Michango na tozo mbalimbali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya WCF, PSSSF na NSSF.

Mhe. Katambi ameyasema hayo Julai 6, 2023 baada ya kutembelea mabanda ya Mifuko hiyo mitatu ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Agizo hilo la Mhe. Katambi linakuja ikiwa ni wiki chache tangu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye wakati akitoa hotuba ya kuahirisha kikao cha Bunge la Bajeti alielekeza ifikapo Septemba 30 mwaka huu, Waajiri kote nchini kutoka sekta ya umma na binafsi wahakikishe wanalipa michango na tozo mbalimbali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Agizo kwa waajiri wote nchini, iwe ni mamlaka za serikali, iwe ni watu binafsi hakikisheni mnapeleka michango, iwe ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), PSSSF au NSSF, mlipe kwa wakati vinginevyo tutachukua hatua kali za kisheria.” Alionya Mhe. Katambi.

Alisema kila mwezi Mamlaka za serikali zinatengewa bajeti ya kutekeleza wajibu huo wa kisheria kuwasilisha michango, hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha wanalipa michango hiyo kwa wakati.

“Kwa sekta binafsi mtu ambaye hawasilishi michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ukimfuatilia vizuri ni mkwepa kodi pia, kwa hivyo inabidi tuwajue vizuri na ikibidi tutawatangaza kwenye (list of shame)”, Alionya Mhe. Katambi.

Aliwapongeza watendaji wakuu wa Mifuko hiyo, Dkt. John Mduma (WCF), CPA. Hosea Kashimba (PSSSF) na Masha Mshomba (NSSF) kwa kuleta mapinduzi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Kwakweli Mhe. Rasi anaona mbali sana hawa wakurugezni wa Mifuko hii, ni watu wa aina yake wameleta mapinduzi makubwa sana kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii, niliwahi kuwakaribisha wageni kutoka Kenya waliokuja kujifunza masuala ya hifadhi ya Jamii kwakweli wameshangaa sana ubora wa huduma zinazotolewa na Mifuko hii.” Alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, Mifuko yote iko vizuri na itaendelea kutoa huduma kwa weledi katika kukusanya Michango na kutoa Mafao, majukumu ambayo wamekabidhiwa na serikali kuyasimamia.

“ Nataka niwahakikishie kuwa tutaendelea kuimarisha eneo la TEHAMA, ulimwengu huu sasa unatoa huduma kwa njia ya TEHAMA, Mifuko yote mitatu inawekeza kwa kasi ili kuhakikisha kwamba sehemu kubwa ya kazi zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao ili kupunguza gharama kwa wateja wetu wawe ni waajiri au wafanyakazi wanaofuatilia Mafao yao.” Alitoa hakikisho Dkt. Mduma

Aidha Mhe. Katambi ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Zanzibar (ZEA) Bw.  Juma Buruhani Mohammed ambaye alisema amefarijika sana kupata fursa ya kujionea shughuli za Mifuko hiyo.

Aliwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Sukuhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mpainduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussen Ali  Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri yanayowezesha ushirikiano mkubwa wa pande zote mbili za Muungano.

Aidha mmoja wa waajiri Bw. Isani Longo kutoka kampuni ya Elfatel Enterprises Company Limited iliyoko Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambaye alifika kwenye banda la WCF kupata elimu ya fidia kwa wafanyakazi alisema yeye ni mmoja wa waajiri ambao Mfanyakazi wake aliumia akiwa kazini na amepata huduma za utengamao kutoka WCF lakini pai amelipwa fidia.

“Mwanzo nilijisajili kwa kutekeleza sheria (compliance) lakini leo nimefika hapa na baada ya kujua kwa undani WCF wanafanya nini, kwakweli nimebaini kuwa kiwango tunacholipa ni kidogo sana cha asilimia 0.5 ya mshahara wa mfanyakazi, ukilinganisha na faida anayopata mfanyakazi endapo atapatwa na madhila akiwa kazini.” Alisema.

Bw. Longo aliwaasa waajiri kutekeza wajibu wa kisheria wa kujisajili kwani kiwango ambacho mwajiri anatakiwa kuchangia ni kidogo sana.

“Kama kila mwajiri akijua kazi ya WCF na dhamira iliyoko mbele, ataona umuhimu wa kutokuwa msumbufu na kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha anajisajili na Mfuko. Alisema.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mhe. Katambi akishuhudia jinsi wanachama wa WCF wanavyohudumiwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post