HALMASHAURI YA MBINGA KUNUFAIKA NA MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI

Katibu Tawala wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Pendo Ndumbaro,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa wadau kujadili rasimu ya Mpango wa matumizi ya ardhi uliondaliwa na mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
Meneja Urasimishaji ardhi ya vijiji kupitia mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Bw. Joseph Osena,akitoa taarifa ya mradi wakati wa Mkutano wa wadau kujadili rasimu ya Mpango wa matumizi ya ardhi uliondaliwa na mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) uliofanyika wilayani Mbinga.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini Mhe. Benaya Kapinga,akizungumza wakati wa Mkutano wa wadau kujadili rasimu ya Mpango wa matumizi ya ardhi uliondaliwa na mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) uliofanyika wilayani Mbinga.

Na Alex Sonna-Mbinga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuupeleka mradi wa Uboreshaji wa Milki salama za Ardhi kwa maeneo ya Vijijini katika Halmashauri saba hapa nchini ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni miongoni mwake.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Pendo Ndumbaro, wakati akifungua Mkutano wa wadau kujadili rasimu ya Mpango wa matumizi ya ardhi uliondaliwa na mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.

Amesema kuwa mradi huo una lengo la kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka ya vijiji na kutumika kama dira ya matumizi sahihi ya kila kipande cha ardhi ndani ya Halmashauri huku ukitoa njia sahihi za kusimamia utunzaji wa maeneo ya hifadhi za vilele vya milima, misitu na vyanzo vya maji.

“Nipende kuchukua fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa jitihada ilizozifanya katika kufanikisha rasimu ya mpango huu wa matumizi ya ardhi.



“Mmeshirikiana vyema na watalaam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mmetoa rasilimali watu na vitendea kazi kama magari na ofisi hata kama mnavyo vichache lakini hamkusita kutoa ili kufanikisha jambo hili”amesema



Aidha, ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi na halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika utekelezaji wa hatua zingine zinazofuata kwenye utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa milki salama za ardhi.



Amesema kuwa hatua hizi ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji, upimaji wa vipande vya ardhi na kutoa hatimiliki za kimila.

“Napenda kushauri kuwa Mpango huu utumike kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka ya vijiji, Mpango huu ukawe dira ya Matumizi sahihi ya kila kipande cha ardhi ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga”amesema Bi.Pendo

Hata hivyo amesema kuwa Mpango huo uanishe na kutoa njia sahihi za kusimamia utunzaji wa maeneo ya hifadhi za vilele vya milima, misitu na vyanzo vya maji pia kuweka maeneo ya kimkakati ya uwekezaji kutokana na rasilimali zilizopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

Amesema kuwa moja ya vipengele muhimu wakati wa utekelezaji wa mradi huo ni kuandaa Mpango wa matumizi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ambao umekwisha andaliwa rasimu na sasa ni zamu ya wadau muhimu wa maendeleo kupitia mpango huo na kutoa maoni yao.



“Pamoja na lengo hilo kuu, uandaaji wa Mpango wa matumizi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya una malengo yenye tija kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa letu kama vile kufungua fursa za uwekezaji, kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka, kuhifadhi mazingira na mwisho kuboresha usalama wa milki za ardhi”amesema

Hata hivyo, amesema Mpango huo ni wa miaka 20 kuanzia mwaka huu 2023 hadi 2043 ukiwa na lengo kuu la kusimamia matumizi ya ardhi na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa watu wanaoishi katika halmashauri ya wilaya kwa kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali ardhi na kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post