DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 75 KUTUMIKA KUJENGA KAMPASI MPYA ZA VYUO VYA UFUNDI NCHINI


Na Mwandishi wetu -Dodoma 

Serikali imetoa Dola za Kimarekani Milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi mpya za vyuo vya ufundi nchini.


Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga Juni 14, 2023 Jijini Dodoma wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo Kipya cha Ufundi cha Dodoma (DTC) kinachojengwa katika eneo la Nala Dodoma.


Naibu Waziri huyo amesema fedha hizo zinakwenda kujenga kampasi mpya ya Chuo cha Ufundi Arusha kinachojengwa eneo la Kikuletwa wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro ambayo itakuwa ikitoa mafunzo ya umahiri ya Uhandisi wa Umeme Jadidifu na kwamba ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2023. Kampasi mbili zinatarajiwa kujengwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ambapo moja itajengwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa wataalam wenye umahiri katika eneo la TEHAMA na Mwanza ambapo itatoa mafunzo ya umahiri katika kuongeza thamani bidhaa za ngozi.



Mhe. Kipanga ameongeza kuwa kampasi nyingine itajengwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya umahiri wa masuala ya usafirishaji katika maeneo ya anga, maji na nchi kavu.


 Amesema kampasi zote hizo zinalenga kuongeza raslimali watu wa kuhudumia maeneo hayo.


"Kazi ya kuandaa rasilimali watu tumekasimiwa sisi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hivyo tutahakikisha tunafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa kwa kuhakikisha kampasi hizo zinakamilika kwa wakati na zinatoa mafunzo yaliyokusudiwa ili taifa lipate wataalam hao" amesisitiza Mhe. Kipanga.


Akizungumzia juu ya Chuo cha Ufundi Dodoma Naibu Waziri amesema kuwa ujenzi wa chuo hicho kitagharimu kiasi cha shilingi bilioni 17.9 ambapo mpaka imeshatumika kiasi cha shilingi bilioni 14.1 na ujenzi umefikia asilimia 95% na kinatarakiwa kukamilika ifikapo Julai mwaka huu.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mhe. Kitila Mkumbo amesema Kamati yake imeridhishwa na kufurahishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia pamoja na ubora wa majengo na kuitaka wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ili mwakani wanafunzi waanze mafunzo.


"Tumefika katika eneo linalojengwa Chuo kizuri sana cha Ufundi Dodoma tumetembelea maeneo mbalimbali tumefurahishwa na hatua ambazo Serikali imechukua ni maono makubwa kwani kitachukua wanafunzi 3000 ujenzi wote utakapokamilika " amesisitiza Prof. Kitila Mkumbo


Prof. Kitila ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kufahamu kuwa kwa sasa ulimwengu unawahitaji kuwa na maarifa na stadi za kazi hivyo vyuo vya ufundi vina anzishwa kwa lengo la kuwapa uwezo na stadi ili waweze kutengeneza ajira zao.


Naye Mkadiria Majenzi wa Chuo cha DTC John Kyara amesema chuo hicho kinajengwa na Mkandarasi CRJE na kwamba ujenzi ulianza June 2021 na kwamba wapo ndani ya muda na mpango kazi na lengo ni kukamilisha kazi kwa wakati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post