KATAMBI: ELIMU YA KANUNI MPYA YA MAFAO ITAENDELEA KUWAFIKIA WAAJIRI NA WANACHAMA
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akijibu swali Bungeni leo Mei 9, 2023, jijini Dodoma.

Na; Mwandishi Wetu: DODOMA

SERIKALI imesema hadi kufikia Februari 28, 2023 wanachama wa mifuko ya pensheni 71,836 na waajiri 2,927 wamefikiwa na elimu ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni (kikokotoo).

Elimu hiyo imetolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo Mei 9, 2023 alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Mhe. Jesca Msambatavangu.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji serikali imejipangaje vipi kushughulikia malalamiko kuhusu kikokotoo.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema serikali ilitangaza matumizi ya kanuni hizo kuanzia Julai mosi, 2022 kupitia Gazeti la Serikali namba 357 toleo la Mei 20, 2022 na kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha, kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko hiyo kuwa endelevu.

“Kwa kutambua wajibu wa kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko pensheni kuhusu kanuni mpya ya mafao ya pensheni, elimu imeendelea kutolewa na mifuko ya pensheni kwa kushirikiana na TUCTA,” amesema.

Amebainisha kuwa mifuko hiyo imetoa elimu kwa waajiri hao ambao 318 ni wanaochangia PSSSF na NSSF ni 2,609 huku wanachama 19,656 wa PSSSF huku NSSF ni 52,180 na kusisitiza elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa kuwa ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku.

Ameongeza kuwa, Serikali ina dhamira njema ya kuwalinda watumishi kwa kuhakikisha wanapata manufaa pindi wanapostaafu ambapo ilifanyika tafiti shirikishi pamoja na tathmini ya mifuko yote kabla na baada ya kuunganishwa kwa kushirikisha kila mdau muhimu, elimu kuhusu Kikokotoo kutolewa kwa uendelevu na Serikali imeiagiza Mifuko ya pensheni iendelee kutoa elimu kwa wanachama wote kabla ya kustaafu, ili kutatua changamoto za mwanachama mmojammoja zinazojitokeza kuhakikisha watumishi wanaostaafu wanalipwa kwa wakati.

Vile vile ameeleza faida ya kanuni mpya ya Kikokotoo kuwa imeweka uwiano na usawa wa mafao baina ya wastaafu wote bila kubagua baadhi ya makundi; Kanuni Mpya imefanya Mifuko kuwa endelevu na kulipa kwa wakati mafao ya Wastaafu; Mafao ya mkupuo yameongezeka kutoka 25% iliyowekwa kwa wanachama wote mwaka 2018 hadi 33%; Malipo ya Mkupuo ya waliokuwa wanachama 1,364,050 (81%) wa Mifuko NSSF, PPF na GEPF yameongezeka na malipo ya pensheni kwa mwezi yameongezeka kwa wanachama 326,137 (19%); na Imeongeza pensheni ya mwezi kutoka 50% ya sasa hadi 67% kwa waliokuwa wanachama wa PSPF na LAPF.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments