TAEC YATUMIA WIKI YA UBUNIFU KUELIMISHA JAMII MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa TAEC Peter Nganilo akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma Katika maonesho ya Wiki ya Ubunifu.


Mtaalamu wa Maabala TAEC Alphonce Mgina akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa habari walipotembelea Banda la tume hiyo kwenye Wiki ya Ubunifu.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

TUME ya nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)imesema inatumia wiki ya Ubunifu  inayoendelea Jijini hapa kutoa elimu kwa jamii juu ya udhibiti wa mionzi kwenye bidhaa na matumizi sahihi ya teknolojia ya nyuklia itakayo linda soko la bidhaa nchini.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa TAEC Peter Nganilo amesema hayo leo Aprili 25,2023 Jijini Dodoma kwenye maonesho ya Wiki ya Ubunifu ambapo ameeleza usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi unaweza kusababisha uchafuzi kwenye vyakula na mazingira.

Amesema TAEC ikiwa na majukumu ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ina wajibu wa kulinda wananchi dhidi ya uchafuzi wa mnyororo wa chakula ikiwa ni pamoja na utafiti na kutoa ushauri na taarifa mbalimbali za sayansi na teknolojia.

"TAEC ndio Mamlaka pekee iliyopewa jukumu la kisheria kudhibiti matumizi salama ya mionzi kupitia maabala maalumu ambapo kiasi cha mionzi iliyoingia  ndani ya mwili wa binadamu hupimwa kulinganisha na kiasi cha mionzi iliyo nje ya mwili wa binadamu,"amesema

Nganilo ameeleza kuwa mionzi iliyoingia kwenye mwili wa binadamu inaweza kuwa imetokana na kumeza au kuingia kupitia njia mbalimbali kwa wafanyakazi wa mionzi au ajali katika sehemu zinazotumia teknolojia ya nyuklia.

"Lengo ni kuona jamii inakuwa salama hivyo kupitia maabala yetu ya kisasa tunapima na kuchunguza sampuli ili kubaini aina na kiasi cha viasili vilivyomo kwa kutumia teknolojia ya nyuklia,"amesema

Amezitaja sampuli zinazopimwa kwenye maabala hiyo kuwa ni  pamoja na za vyakula ,kiteknolojia na kimazingira ikiwemo ,udongo,mimea,hewa,miamba, madini ghafi,mboga mboga,samaki, matunda.

Naye Mtaalamu wa Maabala TAEC Alphonce Mgina ameeleza kuwa Tume hiyo kupitia Maabala yake hupima vyakula vyote vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia mipakani,bandari na viwanja vya ndege Ili kuhakikisha havijachafuliwa na mionzi Kwa kiwango kinachoweza kusababisha madhara Kwa matumizi ya binadamu.

"Aidha tunapima kiasi cha mionzi wanayopata wafanyakazi wa maeneo yenye mionzi kama vile viwandani,migodini,vituo vya utafiti na hospitali ili kuhakikisha usalama wao kwa kuwapatia vifaa vya kuvaa na kuwapatia ushauri wa kinga wakiwa kazini ambapo jumla ya wafanyakazi 2000 nchini wamepatiwa huduma hiyo,"amefafanua 

Mtaalamu huyo wa Maabala amesema TAEC ikiwa imejikita pia katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia hufanya tafiti katika mbegu bora na mazao ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa udongo na mbolea .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post