NAIBU WAZIRI KATAMBI AELEZA SERIKALI INAVYORATIBU WATU WANAOAJIRIWA NJE YA NCHI
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/24, Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 13, 2023.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema serikali imeandaa mfumo maalum wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za watu walioajiriwa nje ya nchi ili kuwaratibu na kusimamia haki zao.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/24, Katambi amesema katika hoja za wabunge kuhusu kuweka kumbukumbu za watu hao tayari umeandaliwa mfumo huo ili wajisajili na kusajiliwa mawakala wa ajira ili kuwa na kanzidata ambayo itasaidia kuwaratibu na kusimamia haki zao.

Aidha, alisema kupitia Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TAESA) na Kamishna wa Kazi wamesajili wakala wa ajira wanaotafuta kazi ndani na nje ya nchi na wanaendelea na majadiliano katika nchi nane ili kuona namna ya kupata fursa za watanzania wengi kuajiriwa nje ya nchi na kutengeneza utaratibu wa kuwasajili waliopo nje ya nchi ili serikali ipate mapato stahiki.

“Kazi zote za nje ya nchi tunataka tusajili vizuri ili kuepusha watanzania wengi kudhalilishwa au kuumizwa au kufanyiwa vitendo visivyofaa nje ya nchi tumeanza kufanyia kazi suala hilo,” amesema.

Kuhusu maendeleo ya vijana, Mhe.Katambi amesema tayari mwongozo wa utoaji mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri sasa kijana mmoja anaweza kupata mkopo kutoka Sh.Milioni 10 hadi 50 huku wenye ulemavu nao wananufaika nayo kwa kuwezeshwa mmoja mmoja kupata mkopo.

“Katika Mfuko wa maendeleo ya vijana tunaendelea kuuboresha ili kuangalia namna ya kuwafikia vijana wengi zaidi kuwasaidia kuwapa mafunzo, kuwatambua walipo na fani zao kuwasajili TAESA na kuwapeleka kwa waajiri ili kupata mafunzo ya utayari wa kufanya kazi, vijana zaidi ya 6,000 wamepelekwa maeneo mbalimbali na wanachangiwa Sh.150,000 na serikali kwa mwezi kwa ajili ya kuwaandaa,” amesema.

Akizungumzia Watu wenye Ulemavu, Mhe.Katambi amesema Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan amesaidia kufufua vyuo vya watu wenye ulemavu na utegamao vilivyokuwa havifanyi kazi kwa zaidi ya miaka 10 na tayari baadhi vimeanza kutoa mafunzo.

Kuhusu ukusanyaji wa maduhuli, Naibu Waziri Katambi amesema mkakati umeandaliwa wa kuangalia namna ya kutekeleza hilo ambapo magari 17 yanatarajiwa kupatikana ili kufanya ukaguzi maeneo ya kazi na kuhakikisha kuna kazi za staha na usalama mahali pa kazi.

Kuhusu kuongeza bajeti katika Programu ya Kukuza Ujuzi, Naibu Waziri huyo amesema lengo la dira ya maendeleo ya taifa ifikapo mwaka 2025 inakusudia kutoa mafunzo kwa watanzania zaidi ya 681,000 ndani ya miaka mitano.

“Tayari Wizara ya Fedha imejizatiti kutoa fedha ili kuhakikisha mafunzo haya yanafanyika lakini kumekuwa na program mbalimbali za ukuzaji ujuzi kwa mwaka 2021/22 tulipata zaidi ya Sh.Bilioni tisa ambazo zilikwenda kuwasaidia vijana wengi wa kitanzania kupata mafunzo,”amesema.

Aidha, amesema suala la kushirikiana na wadau kutoa programu za mafunzo wapo wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na serikali ikiwamo GiZ, ILO, IOM katika masuala ya kibajeti ili watanzania wapate fursa ya mafunzo hayo ya kukuza ujuzi na kuwaandaa kukabiliana na soko la ajira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post