BENKI YA CRDB YAFUTURISHA WATEJA NA WADAU NA KUTOA CHAKULA KWA WATOTO YATIMA TABORA….RC BATILDA APONGEZA HUDUMA YA AL BARAKAH BANKING

Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Ndg. Jumanne Wambura Wagana akizungumza wakati Benki ya CRDB ikiwafuturisha Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tabora

Na Mwandishi Wetu – Malunde 1 blog Tabora

Benki ya CRDB imewafuturisha Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tabora ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wa Benki hiyo kuungana na Waumini wa Dini ya Kiislamu wanaoishiriki Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB imefanyika Jumatano Aprili 5,2023 katika Hoteli Ya Ristalemi na kuhudhuriwa na viongozi wa dini, Viongozi wa Serikali, Taasisi za Umma na Binafsi, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa,Viongozi na Wafanyakazi kutoka Benki ya CRDB, Watoto yatima na wateja na wadau wa Benki ya CRDB ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani.

Akizungumza wakati wa Futari hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani ameipongeza Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kuanzisha na kuendeleza utaratibu huo wa kufutari na wateja, wadau na wenye uhitaji katika jamii katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Nimefurahishwa na jambo mlilolifanya leo la kutoa msaada wa fulana na kofia kwa Watoto wenye uhitaji maalum katika Shule ya Furaha, hakika lile ni jambo la kuigwa. Nimekuwa nikiwafuatilia kwa muda na kuona namna gani ambavyo mmekua mkitekeleza jambo hili na niliona mwaka huu mlianza jambo hili kwa kufuturu na wateja wa Dar es Salaam mkiongozwa na Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania. Hongereni sana”, amesema Dkt. Batilda.


“Ushiriki wenu katika kuandaa futari hizi katika mwezi Ramadhani inaonesha ni kwa jinsi gani Benki ya CRDB inatambua kuwa pamoja na kufanya biashara lakini ni sehemu ya jamii na inapaswa kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii. Hakika hili ni jambo jema linalopaswa kuigwa na taasisi nyingine ambazo ni sehemu ya jamii yetu”,amesema.


Aidha pamoja na mazuri hayo ambayo Benki ya CRDB wamefanya kwa kushiriki na wateja na wadau wao katika futari, Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Benki hiyo kuanzisha huduma makhususi za Al Barakah Banking ambazo zinafuata misingi ya dini ya Kiislamu.


“Hakika hii inadhihirisha kuwa CRDB ni Benki inayomsikiliza Mteja kwani mmeweza kutambua mahitaji ya kundi lenye uhitaji wa huduma zinazofata misingi ya dini ya Kiislamu na kuweza kubuni huduma zinazoendana na mahitaji yao.Mafanikio ya huduma ya Al Barakah yatanufaisha sio tu Benki ya CRDB kwani kwa kuanzisha huduma hii mmeweza kuwajumuisha watu ambao mwanzo wasingeweza kujumuishwa katika huduma rasmi za kibenki kwa kuwa huduma zilizokuwepo zilikua haziendani na misingi ya imani yao”,amesema Dkt. Batilda.


“Hivyo kwa kuwajumuisha watu hawa mana yake mmeongeza wigo wenu wa kupokea amana na kwa sababu hiyo mtaweza kutoa mikopo zaidi kwa wafanyabiashara nchini na hivyo kutoa ajira zaidi, kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa pamoja na uwekezaji kwa ujumla wake.

Hivyo kama Mkuu wa Mkoa, nafurahishwa na jambo hili kwani kwa namna moja au nyingine mmtakuwa na mchango katika kutimiza majukumu yangu ya kumsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuyafikia makundi yote yaliyopo katika jamii”, ameongeza Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora.

Akitoa salamu za benki ya CRDB, Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Ndg. Jumanne Wambura Wagana amesema benki hiyo imekuwa na utaratibu huo kila mwaka wakati wa Ramadhan kushiriki Futari na wateja wake na kutoa Sadaka ya vyakula kwa watoto yatima.


Wagana amesema mwaka 2021 benki ya CRDB ilianzisha dirisha la huduma za kibenki ambazo zimefuata misingi ya dini ya kiislamu maarufu kama Al Barakah Banking ambapo mpaka mwaka 2022 benki hiyo imeweza kupata wateja zaidi ya 30,000 na kutoa mikopo isiyo na riba kwa wateja wake kwa kiasi zaidi ya Shilingi Bilioni 73.


Amesema kwa Kanda ya Magharibi yaani Shinyanga, Geita, Kigoma na Tabora amesema mkoa wa Tabora umepokea huduma hiyo mpya ya Al Barakah kwa kasi zaidi hivyo kuwaomba watanzania ambao hawajajiunga wachangamkie fursa kwani ukiweka amana kwa akaunti ya Al Barakah haitengenezi riba na pia ukipewa mkopo hauna riba.

Wagana amewapa uhakika wa huduma wateja wote ambapo amesema benki hiyo kinara nchini yenye kauli mbiu ya benki inayomsikiliza mteja kwa sasa imeendelea kuzifanya huduma zake zipatikane kidigitali zaidi ikiwemo kupitia Mawakala, ATM, Simbanking, Vituo vya malipo n.k huku ikiendelea kupanua mtandao wake nje ya Tanzania ambapo kwa sasa CRDB inafanya vizuri nchini Burundi kama benki namba 2 na hivi karibuni wanatarajia kuanza kutoa huduma nchini Congo.


Mkurugenzi wa NBS na MNEC Tabora Mhe. Mohamed Nasson naye ameguswa na kitendo cha CRDB kutoa sadaka ya vyakula kwa watoto yatima akatoa Tsh 250,000/= huku mkuu wa Mkoa Dkt. Batilda Buriani naye akiguswa na kuongezea Tsh 250,000/= na kufanya iwe 500,000/= ambapo fedha hizo zitakabidhiwa kwa viongozi wa kituo cha kulelea watoto yatima ili wanunue mahitaji kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akizungumza wakati Benki ya CRDB ikiwafuturisha Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tabora
Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Ndg. Jumanne Wambura Wagana akizungumza wakati Benki ya CRDB ikiwafuturisha Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tabora

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post