WANANCHI MWAMANYUDA WACHANGA SARUJI UJENZI WA SHULE YA MSINGI...."WATOTO WANATEMBEA UMBALI MREFU KWENDA SHULE"


Diwani wa Kata ya Imesela, Seth Msangwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
Diwani wa Kata ya Imesela, Seth Msangwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
Sehemu ya wakazi wa Kijiji cha Mwamanyuda Kata ya Imesela wakiwa kwenye mkutano wa hadhara

Na Halima Khoya,Shinyanga.

Wakazi wa Kijiji cha Mwamanyuda Kata ya Imesela Wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali kuunga mkono jitihada za wananchi waliojitolea kujenga shule ya msingi Magugushi ili kuwaondolea watoto wao adha ya kutembea umbali mrefu hali inayosababisha kufeli kwenye masomo yao na kuchangia vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Wakizungumza kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 26 Mwaka huu, Wakazi hao wamesema kijiji hicho kina vitongoji vinne (4) ambavyo vinatumia shule mbili za msingi (Kihongwe na Mwamanyuda) na kusababisha watoto wawe watoro kutokana na kutembea umbali mrefu.


Wananchi hao wamesema watoto wanaosoma Shule ya msingi wanatembea kilometa nyingi ambapo wakichoka kutembea hulala na wengine kuishia njiani na kurudi nyumbani hali inayowakosesha haki ya kupata elimu.


Hata hivyo wananchi hao wameafikiana kuchangia kwa ajili ya ujenzi huo kwa kutoa mfuko mmoja wa saruji kwa kila kaya ambapo kwenye kijiji kuna jumla ya kaya 333 ambazo zimegawanyika kwa vitongoji (kitongoji cha Mizanza kina kaya 96,Mwambenghene kaya 61,Mwantarika kaya 56 na Magugushi kaya 120) na mchango unaanza kutolewa Februari na kumalizika Mei 2023 ili kuanza ujenzi.


“Nimelipokea kwa asilimia mia kwa sababu watoto wetu wanatembea umbali mrefu,mwishoni wanalala njiani na wengine kurudi nyumbani, serikali tunaiomba ituunge mkono jitihada”, amesema Ester Peter.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Imesela, Seth Msangwa amewataka wananchi kuwa wavumilivu kusubiria tume ya ardhi kutoka Halmashauri ya Shinyanga itakayowaruhusu kuanza ujenzi huku akibainisha kuwa kukamilika kwa Taasisi hiyo ya elimu itasaidia kusogezewa huduma za kijamii (Maji,barabara na umeme).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments