GGML, GEITA WAJIVUNIA NYANKUMBU SEKONDARI KUNG'ARA MATOKEO KIDATO CHA NNE


Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyankumbu wakijisomea maktaba (library). Shule hii ya wasichana ni ya mfumo wa sayansi na inawanafunzi zaidi ya 1050, imesheheni vifaa vya maabara, nyumba za kisasa 36 kwa ajili ya walimu, madarasa 21 na viwanja mbalimbali vya michezo. Pamoja na miradi mingine ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, GGM imewekeza Sh bilioni 10 katika ujenzi wa shule hii kubwa na ya kisasa.


Na Mwandishi wetu - Geita

WAKATI wakuu wa mikoa na wilaya wakihaha kuhamasisha wazazi wawapeleke watoto wao shule kujiunga na kidato cha kwanza, kwa upande wa Shule ya sekondari ya Wasichana Nyankumbu imezidiwa kwa wingi wa maombi ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule hiyo kutokana na ufaulu mzuri na mazingira mazuri ya kujifunzia.


Shule hiyo ya Serikali, ilijengwa na kuzinduliwa mwaka 2014 na Kampuni ya Geita Gold Miningi (GGLM) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kupitia fedha za mfuko wa uwajibika wa kampuni kwa jamii, imetajwa kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa kike katika mkoa huo.


GGML ilitumia jumla ya Sh bilioni 15 katika ujenzi wa shule hiyo ya bweni pamoja na kuboresha miundombinu ya shule nyingine za mkoa huo ikiwamo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuborsha sekta ya elimu nchini.


Akizungumza na mwandishi wetu jana, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Georgia Mugashe alisema katika mwaka huu wa masomo imesajili wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza 240 huku ikishindwa kuchukua wengine kutokana na wingi wa maombi.


Alisema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 1,050 imekuwa mkombozi kwa jamii ya wanaGeita kutokana na mwenendo mzuri wa matokeo ya shule katika mitihani ya kidato cha nne sambamba na mazingira mazuri ya kusomea ikiwamo miundombinu bora iliyojengwa na GGML.


Alibainisha kuwa kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2022, wanafunzi wote wamefaulu na hakuna haliyepata daraja sifuri.


“Jumla ya wanafunzi 38 walipata daraja la kwanza, 86, daraja la pili, 36 daraja la tatu na sita daraja la nne. Kwa hiyo unaona namna tunavyopambana kuhakikisha wote wanapata daraja la kwanza kwa sababu hata katika matokeo yam waka juzi yaani 2021, waliopata daraja la kwanza walikuwa 50.


“Tunawashukuru sana GGML kwa sababu huwezi kuamini hii ni shule ya serikali kutokana na huu mwamko wa wazazi kuleta watoto wao hapa. Na hakuna kingine zaidi kinachowavutia, ni ufaulu mzuri na mazingira mazuri ya kusoma, kwani wazazi hupenda watoto wakae bweni,” alisema.


Aidha, alisema kutokana na mwamko huo, idadi ya wanafunzi imeongezeka hadi shule kuzidiwa kwani mabweni yaliyopo sasa hayatoshi.


Amewaomba wadau pamoja na watu wengine kujitokeza kuendelea kuunga mkono Serikali na GGML katika kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Akizungumzia matokeo hayo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema inafurahisha na kutia moyo kuona shule ambayo GGML imeianzisha kwa lengo la kuboresha elimu mkoani Geita ikifanya vizuri na kuwa kivutio kwa wazazi.

Alisema GGML imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali kwani pia imejenga miundombinu katika shule za Bugando na Kamena ambazo zimeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 2021/2022.

“Jumla kwenye shule hizi mbili tulitumia Sh milioni 287.5 na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita, fedha hizi zilitolewa kupitia mfuko huo wa wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR),” alisema.


Naye Mwenyekiti wa bodi ya shule kwa upande wa wazazi, Eliangikaya Mshana pia aliishukuru GGML kwa kuendelea kuungana na wazazi pamoja na jamii ya Geita kuboresha mazingira ya elimu mkoani humo hadi kuwezesha shule hiyo kuwa moja ya shule ya mfano katika mkoa wa Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments