ALIYEIBA MALI ZA MAREHEMU AJIUA MAHABUSU POLISI



Mtuhumiwa mmoja kati ya 14 waliokamatwa wakihusishwa na uporaji mali za abiria waliofariki na kujeruhiwa katika ajali ya basi dogo aina ya Coaster na lori aina ya Fusso Februari 4, amedaiwa kujinyonga katika mahabusu ya Polisi jijini Tanga.


Basi hilo lilikuwa likisafirisha msiba kutoka Dar es Salaam kuelekea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na ndipo lilipogongana na Fuso katika kijiji cha Magila wilayani Korogwe mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu 20 katika eneo hilo na wengine kufia hospitali.


Kufuatia ajali hiyo, baadhi ya watu waliodaiwa kupora mali katika eneo hilo walikamatwa.


Akizungumza wakati akishuhdia utiaji saini wa miradi 51 ya maji yenye thamani ya Sh41 bilioni leo Februari 23 jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba amesema mtuhumiwa mmoja kati ya wanane waliokuwa wakishikiliwa na Polisi amekutwa amejinyonga usiku wa kuamkia Alhamisi.


Amesema awali walikamatwa watuhumiwa 14, lakini watuhumiwa sita waliachiliwa baada ya kufanyika mchujo.

Mgumba amesema, mtuhumiwa aliyejinyonga ni ambaye wakati wa upekuzi uliofanywa na polisi nyumbani kwake kulikutwa na baadhi ya vitu zikiwamo simu, begi na nguo vikiwa na alama za damu.


"Mtuhumiwa aliyejinyonga ni yule ambaye wakati wa upekuzi nyumbani kwake kulikutwa na baadhi ya vitu vikiwa na alama ya damu kama simu, begi na nguo zinazoshukiwa kupora kwenye eneo la ajali,” amesema.




Jeshi la polisi limeahidi kutolea maelezo tukio hilo mara baada ya kukamilika uchunguzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments