MWAMALA WALIA CHANGAMOTO YA MAJI.... "TUNATUMIA MUDA MREFU KUFUATA MAJI, TENA YANA CHUMVI MATUMBO YANAUMA"

 


Mtoto akichota maji katika moja ya visima kitongoji cha Wela kijiji cha Mwamala B kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa kitongoji cha Wela kijiji cha Mwamala B kata ya Mwamala, Bw. Giti Singu Giti akionesha kisima cha maji kinachotumiwa na wananchi.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wakati dunia ikiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia bado wananchi wa kata ya Mwamala katika mkoa wa Shinyanga wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji hali inayosababisha kutumia muda mrefu kufuata huduma hiyo ya maji ambayo pia yana chumvi.

Wakizungumza na Malunde 1 blog iliyotembelea kata hiyo, wananchi hao wamesema ukosefu wa maji safi na salama unawalazimu kutumia maji ya chumvi wenye visima walivyochimba pembezoni mwa mito ambayo si salama na wamekuwa wakitumia zaidi ya dakika 30 kufuata maji hayo kwa baiskeli na kujitwisha kichwani zaidi ya saa moja kwenda tu.

“Changamoto ya maji ni kubwa hapa Mwamala, tunalazimika kutumia maji ya chumvi kwenye visima vilivyo pembezoni mwa mto, maji haya ya chumvi siyo salama kwa afya kwani ukiyanywa tumbo linauma. Wanawake wanatumia muda mrefu sana kufuata maji badala ya kufanya shughuli zingine za kujiingizia kipato. Tunaomba serikali ituletee maji ya ziwa Victoria kwani ahadi zimekuwa nyingi sana”,amesema Bw. Nkende Mabula.

Naye Bi. Nyamizi Manoni amesema endapo serikali itawasogezea huduma ya maji wataweza kujishughulisha na kazi za kujiingizia kipato badala ya kutumia muda mrefu kutafuta huduma ya maji akieleza kuwa mfano hulazimika kuamka saa 12 kufuata maji na kurudi saa nne asubuhi kutokana na foleni kubwa ya wananchi wanaosubiri huduma ya maji hayo licha ya kwamba ni ya chumvi.

Kwa upande wake, Bi. Mhoja Masali kutokana na changamoto hiyo ya maji, wakati mwingine wanalazimika kusafiri kwa zaidi ya saa mbili kufuata maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Mwawaza hivyo kuiomba serikali kuwaonea huruma kwani wanawake ndiyo wanahangaika zaidi na wakati mwingine kusababisha migogoro ndani ya ndoa hivyo kuchochea ukatili wa kijinsia.

“Kwa kweli maji ni shida hapa Mwamala, mimi nina umri wa miaka 77, tumekuwa tukitumia maji yasiyo salama, tunatumia pamoja na mifugo kwenye mto Wela ambako huwa tunachimba visima pembezoni mwa mto. Haya maji ni ya chumvi”,amesema Mboje Malale.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Wela kijiji cha Mwamala B kata ya Mwamala, Bw. Giti Singu Giti amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji na kueleza kuwa wananchi wamekuwa wakihangaika kufuata maji ya chumvi kwenye visima vilivyopo kwenye maeneo yao na mtoni.

 Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala Halmashauri ya Shinyanga Bi. Suzana Kayange amesema ni kweli katika kata hiyo kuna changamoto ya maji na hasa kipindi cha kiangazi kumekuwa na uhaba mkubwa wa maji hali inayopelekea kufuata maji ya kunywa kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga huku wengine wakitumia maji ya chumvi na ya kwenye madimbwi.

Hata hivyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wanaendelea na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kuboresha visima vilivyopo pamoja kuleta Maji ya Ziwa Victoria.

“Shirika la Life Water International kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),wananchi wanajenga kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Bugogo lakini pia kutajengwa mradi wa Maji ya Ziwa Victoria katika vijiji vya Mwamala B na Ibanza kupitia fedha za Benki ya Dunia”,amesema Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala.

Akizungumza na Malunde 1 blog, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Shinyanga Mhandisi Emael Nkopi amesema RUWASA kwa kushirikiana na Shirika la Life Water International na wananchi wanaendelea na ujenzi wa mradi wa maji ya kisima kirefu katika kijiji cha Bugogo.

“Tayari katika Kijiji cha Bugogo tumechimba kisima kirefu cha maji kwa kushirikiana na Life Water International na wananchi, mtandao wa bomba, tunatarajia Life Water International ikipata pesa mapema utajengwa kuanzia Januari 2023”,amesema Mhandisi Nkopi.

“Pia tunaendelea na ujenzi wa mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kupitia Mkandarasi Mbeso Construction unatakaonufaisha vijiji vinane katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambavyo ni Masengwa, Ishinabulandi,Mwamala B, Bubale,Idodoma, Isela, Ibingo, Ng’wanghalanga na sehemu ya kijiji cha Ibanza. Tunatajia kukamilisha ujenzi wa mradi huu katika mwaka wa fedha 2022/2023 na tayari ujenzi wa tanki la maji kijiji cha Mwamala B unaendelea”,ameongeza Nkopi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post