WADAU WA MAENDELEO WATAKA JAMII KUUNGA MKONO JUHUDI ZA VIJANA KATIKA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

 


Waziri wa elimu, sayansi na Teknolojia Prf.Adolf Mkenda akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa kampuni ya habari ya Wazo Huru yenye makao yake makuu Jijini Dodoma .


Na Dotto Kwilasa,DODOMA.


BAADHI ya wadau wa Maendeleo nchini wameitaka jamii kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vijana katika kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwakatisha tamaa.


Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kampuni ya habari ya Wazo Huru  inayomilikiwa na mwandishi wa habari mwandamizi Mathias Canal na kueleza kuwa juhudi za vijana ni hazina kwa uchumi wa taifa .


Mmoja wa wadau hao ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda  amesema vijana wa kitanzania wanapaswa kuwa wabunifu na  kujenga utamaduni wa kusaidiana na kuvushana katika vikwazo vinavyo wakwamisha ili kufikia ndoto zao.


Amesema hali hiyo itawasaidia kukua na kuwa na uwezo wa kujiajiri hali itakayo isaidia Serikali kupunguza kundi la watu wasio na ajira.

 

Waziri Mkenda amesema kwa sasa Serikali imepiga hatua kubwa katika kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kwamba kupitia uzinduzi wa kampuni hiyo inayojihusisha na masuala ya habari itasaidia kuajiri vijana wengi wenye maono.


"Huyu ni kijana wetu,Mtanzania mwenzetu ameweza kuunga mkono juhudi za Serikali Katika masuala ya uwekezaji,Katika uwekezaji wake huu mdogo ameongeza chachu kwa vijana wengine kuona ni namna gani wanaweza kuajiriwa na kuajiri vijana wengine,"amesisitiza 

 

Waziri Mkenda pia amesema,"Sisi watanzania tunapaswa kuongeza bidii ya kufurahia mafanikio ya wenzetu, tukiona mwenzetu mwenye ndoto anafanikiwa tunamuunga mkono kwa kumuombea na sio kukatishana tamaa,"alisema

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Mhandisi Mathew Kundo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa WazoHuru kwa hatua hiyo huku akimtaka kuhakikisha anafuata sheria na Kanuni za uandishi wa habari kwa kufuata matakwa ya kisheria.


"Kuna miiko ya taaluma ya habari ,ili ufanikiwe lazima ukubali kuiishi,hatutegemei kuona unakiuka kama wengine,na hapo utakuwa umesaidia taifa kupitia maudhui yako;


Baada ya mapinduzi ya teknolojia badala ya kusubiri taarifa kwenye televisheni ya nyumbani sasa tunaruhusu watu kuwa na televisheni ya mtandaoni na mwananchi anaweza kupata habari kupitia simu yake ya mkononi, tumeshuhudia leo umezindua televisheni ya Mtandaoni ni jambo kubwa kama wizara tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha" amesema

 

Ameongeza kuwa amefurahishwa na kuona kijana wa kitanzania anajiajiri na kuweza kuajiri vijana wengine ili kuhakikisha wanajipatia kipato na kuwezesha upatikanaji wa habari na elimu kwa jamii kwa urahisi.

 

Akitoa taarifa ya kampuni hiyo, Mtendaji Mkuu Mathias Canal ameiomba Serikali kuona namna ya kuwawekea mazingira mazuri vijana Wenye taaluma  ya Habari na mawasiliano Katika kujiajiri kwa kumiliki vyombo vya habari ambavyo vitarahisisha upatikanaji wa taarifa za kitaalamu na ujuzi kwa jamii.

 

Ameongeza kuwa mpango wa kampuni hiyo iliyojipambanua katika masuala ya Habari na mawasiliano ilianza kupitia kundi la WhatsApp Mkoani Iringa mwaka 2014 na baadae kuanzisha televisheni ya Mtandaoni (Youtube Tv) pamoja na Blog.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments