CCM YASIMAMISHA UCHAGUZI SIMIYU, MBEYA, ARUSHA

 
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesimamisha uchaguzi katika mikoa mitatu kwa nafasi zilizoonyesha kuwa na changamoto pamoja na kufuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho Kutokana na sababu za rushwa .


Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kuongeza kuwa  baada ya tukijiridhisha kama hakutakuwa na  changamoto ,chama kitaruhusu  uchaguzi kufanyika na kama watabaini  changamoto wataondosha wagombea wenye changamoto na wasio na changamoto kuendelea na uchaguzi kwa nafasi husika.


Amesema baada ya uchunguzi wa kina wa changamoto katika maeneo husika ,hatua zaidi zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wahusika kugombea na kisha kuwakabidhi katika vyombo vyenye dhamana ya kufuatilia masuala ya rushwa.


“Mikoa ambayo tumefanya  uamuzi ni pamoja na kufuta uchaguzi wa umoja wa Vijana mkoa wa Simiyu , pia tumesimamisha uchaguzi wa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mbeya kwa sababu ya tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa ambako nako tunafanya uchunguzi wa kina tukikamilisha tutatoa taarifa ya uamuzi wa chama,"amesema Chongolo.


Pamoja na hayo amesema," tumesimamisha uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM  mkoa wa Arusha kwa sababu hiyo hiyo ya rushwa na  tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa za uamuzi wa chama ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi kuendelea".


Katibu Mkuu huyo pia amezungumzia kuhusu tukio la wanachama kuondoka na boksi la kura katika uchaguzi uliofanywa jana (juzi)  mkoa wa kichama wa Magharibi Zanzibar na kueleza kuwa watu hao walienda na boksi hilo kwenye chumba kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuhesabia kura .


 “Sasa  tunataka kuangalia uchukuaji wa boksi hilo ulilenga kuhesabu kura au ulikuwa una lengo lingine,tutafuatilia tukijiridhisha tutachukua uamuzi ukiwemo kuufuta uchaguzi na kurudiwa upya ili kutenda haki ,tukijiridhsisha kwamba lengo la  kuchukua boksi hilo ulilenga kwenda  kuhesabu kura basi tutaruhusu matokeo ya uchaguzi huo yaendelee kama yalivyo.”amesema


Aidha Chongolo amezungumzia kuhusu changamoto iliyopo sasa ndani ya chama hicho kuwa ni kuwepo kwa wajanja  wachache wanaogombea nafasi mbalimbali au wapambe wao kutengeneza msukumo wa kuonyesha wao ni maalum kuliko wengine  na wao ndio wanaotakiwa na viongozi wa juu kuliko wengine.


“Wapo humu wengine wanajiita wagombea wa katibu Mkuu ,wapo wanaojiita wagombea wa Makamu Mwenyekiti ,wengine wanajiita wagombea wa Mwenyekiti na wapo wanaojiita wagomeba wa wajumbe wa kamati kuu,sisi tulishapitisha majina,na  kama tumepitisha kwenye mkoa majina matatu ,moja ,mawili au manne na kuendelea maana yake hao ndiyo wagombea wa chama,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments