WAFANYAKAZI OWMS WATAKIWA KUWEKA MAHALA PA KAZI KUWA SEHEMU SALAMA


 
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akizungumza na wajumbe wa Baraza la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza kwa wajumbe wa Baraza jipya wa Ofisi hiyo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA


Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kutumia mafunzo wanayopatiwa kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza la wafanyakazi katika kuweka mahala pa kazi kuwa sehemu salama.

Dkt. Luhende ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wapya wa Baraza la Wafanyakazi wa OWMS yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ambapo amesema mada tatu zitawasilishwa kwa wajumbe hao ikiwemo Wajibu na Majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi; Kupitia Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi; na Umuhimu wa Baraza la wafanyakazi mahala pa kazi.


Amewataka wajumbe kutumia fursa hiyo kuzijua hadidu za rejea ambazo zitawaongoza katika utendaji kazi wa kila siku na kutekeleza majukumu katika kipindi chote cha miaka mitatu watakachokuwa wajumbe wa Baraza hilo kuwa nguzo kati ya Baraza na watumishi wengine kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu mahala pa kazi na kuwa sehemu salama ili kuleta tija katika utendaji kazi wa kila siku wa OWMS na amewataka wajiandae kuhamia Dodoma mwaka huu.


“Mada inayohusu Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi ni mahususi kwa ajili ya kujenga uwezo na maarifa ya kujua kilichopo katika mkataba wetu kati ya Menejimenti na Baraza hili ikiwemo matarajio ya OWMS kutoka kwa wajumbe ukizingatia kuwa mkataba huu ni nyenzo muhimu kabisa katika utendaji kazi wetu kwa sababu unaainisha majukumu na mipaka yetu na matarajio kutoka kwa wafanyakazi,” amesema Dkt. Luhende.


Akitoa mada ya Umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samuel Nyungwa amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi kujiunga na chama cha wafanyakazi kwa sababu ni taasisi pekee ya wafanyakazi ambayo imeundwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki kwa kuweka sawa mahusiano ya kazi kati mfanyakazi na mwajiri wake mahali pa kazi.


“Vyama vya wafanyakazi ni wadau muhimu sana katika kulinda, kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi katika kuchangia jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba ustawi wa raia wake ambapo ni wafanyakazi unaboreshwa na utendaji kazi unasimamiwa,” amesema Nyungwa.


Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sebastian Innosh amewasilisha mada kuhusu umuhimu na uendeshaji wenye tija wa mabaraza la wafanyakazi ambapo amesema kuwa mabaraza yanatakiwa kushauri na kujadili masuala muhimu ya taasisi; kutumia rasilimali watu na fedha kwa manufaa na uendelevu wa taasisi husika na taifa kwa ujumla; na kuimarisha mahusiano mema na kudumisha amani na utulivu mahala pa kazi.


Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemarila Rutatina amesema kuwa mkataba wa Baraza la Wafanyakazi unaleta mafanikio na ushirikiano mahala pa kazi kwa kuwa unawaweka pamoja na kuwaleta karibu watumishi mahali pa kazi.


Akitoa maoni yake wakati wa mkutano huo, Athuman Zunda ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo la OWMS amesema kuwa wamejifunza masuala mbalimbali kuhusu muundo wa Baraza hilo na idadi ya wajumbe wake kwa kuwa yeye ni mjumbe kwa mara ya kwanza kwenye Baraza hilo hivyo wamejifunza na kufurahishwa na namna ambavyo uongozi wa Baraza unavyofanya kazi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post