TAASISI YA AFRIKA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA YA NELSON MANDELA KUINGIZA SOKONI MFUMO WA KUBAINI MACHAPISHO YA WIZI

 
Makamu Mkuu wa Chuo, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) leo Oktoba 20,2022 jijini Dodoma kuhusu shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

MAKAMU Mkuu wa Chuo, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga
amesema wapo katika hatua za mwisho kuingiza sokoni mfumo wa kubaini machapisho ya wizi ambapo mfumo uliokuwa ukitumika katika vyuo vingi ni wa kutoka nje na wa gharama kubwa.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 22,2022 jijini Dodoma na Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof.Emmanuel Luoga,wakati akitoa taarifa  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Prof. Luoga amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika matumizi ya TEHAMA ambapo itapata Dola za Marekani milioni 10 mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, fedha hiyo itatumika kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha inapata ithibati ya maabara ya viwango vya kimataifa.

“Taasisi imejikita katika kuboresha ufundishaji kwa kutumia teknolojia ya masafa (e-learning) kwa waadhiri na kupanua wigo kwa wanafunzi walio mbali na kampasi kupata elimu ya masafa,”amesema Prof.Luoga

Amesema kuwa mpaka sasa taasisi imefanya bunifu 73 ambazo ni matokeo ya ushirikiano wa hali ya juu kati ya wahadhiri na wanafunzi pamoja na Serikali na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi. 

“Katika masuala ya utafiti na ubunifu, mpaka sasa taasisi yetu imefanikiwa kufanya bunifu 73 ambazo ni matokeo ya ushirikiano wa hali ya juu kati ya wahadhiri na wanafunzi pamoja na Serikali na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi,”Amesema Prof.Luoga

Prof.Luaga amesema kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine mbili wanaanzisha Kituo cha Umahiri cha Ndizi ambacho kitahusika na masuala ya utafiti wa mbegu, namna ya kuongeza tija katika upandaji na usimamizi wa zao la ndizi na matumizi bora. 

Aidha amesema Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imeidhinisha bajeti ya takriban Shilingi bilioni 43 kwa ajili ya taasisi hiyo ambapo  kipaumbele kikubwa ni ujenzi wa bweni maalum kwa ajili ya wanachuo wanawake wenye mahitaji maalum na wenye watoto wadogo ambao mradi huo  tayari umeshaanza tangu Oktoba, 2021 na kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kimeshatumika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo  na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali inafanya kazi kubwa kuandaa wanasayansi kutoka shule za msingi mpaka shahada za kwanza ambapo kwa sasa inajenga shule moja ya sekondari ya masomo ya sayansi kwa kila mkoa kwa ajili ya wasichana. 


"Nitoe wito kwa vyuo mbalimbali nchini kuweka kozi za umahiri kwa Waandishi wa Habari ili wakafanye tafiti za kutosha, hivyo kuondokana na kutoa habari za uongo na zisizokuwa na tija kwa umma,"amesema
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post