KAMPASI YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KUJENGWA KAGERA-Prof. MKENDA

 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda.

 Na Mwandishi wetu,Kagera.

KATIKA kuboresha huduma za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi nchini,Serikali imejipanga kujenga Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Mkoani Kagera.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema hayo mbele ya Mgeni rasmi-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan tarehe 13 Octoba 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chuo kipya cha Ufundi Stadi na Huduma (VETA) cha Mkoa wa Kagera.

Amesema kuwa Kampasi hiyo itajengwa kwenye vijiji vya Itahwa na Kangabusharo kwenye eneo la ekari 323.45. Kati ya ekari 323.45 zilizotolewa, ekari 231.36 ziko katika kijiji cha Itahwa na ekari 92.09 katika kijiji cha Kangabusharo. 

Akizungumza kuhusu Chuo kipya cha Ufundi Stadi na Huduma (VETA) cha Mkoa wa Kagera, Waziri Mkenda amesema chuo hicho chenye hadhi ya Kimataifa kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa thamani ya Yuani za Kichina Milioni 60.18 sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 22.4, Fedha hizo zinajumuisha shughuli za ujenzi, uwekwaji wa baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mashine na samani katika majengo.

Waziri Mkenda amesema kuwa Chuu hicho chenye karakana, vifaa na miundo mbinu ya kisasa kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1,400 kwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika fani mbalimbali za ufundi na huduma.

Waziri Mkenda amesema kuwa Chuo hicho cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera kilichozinduliwa na Mhe Rais ni hatua nyingine muhimu katika mpango wa kukamilisha ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya ngazi ya Mikoa. 

“Mheshimiwa Rais Tulibakisha mikoa michache sana. Kwa sasa, mikoa mingine ambayo ujenzi unaendelea ni Njombe, Simiyu, Rukwa na Geita na mpango wa ujenzi wa chuo cha Mkoa wa Songwe unaendelea kukamilishwa ili ujenzi uanze” Amekaririwa Prof Mkenda 

Prof Mkenda amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya ngazi ya wilaya ambavyo hadi sasa Wilaya 77 zina vyuo na ujenzi wa vyuo katika Wilaya 62 unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha 2022/23 ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni 100. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post