TGNP YAPONGEZA KIKOSI KAZI KILICHOUNDWA NA RAIS SAMIA KWA KUZINGATIA SUALA LA USHIRIKI WA WANAWAKE NA MAKUNDI YALIYO PEMBEZONI KATIKA SIASA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi


 TAMKO

PONGEZI KWA KIKOSI KAZI CHA KURATIBU MAONI YA WADAU WA DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI KWA KUWASILISHA MAPENDEKEZO YALIYOZINGATIA KUONGEZA USHIRIKI WA WANAWAKE NA MAKUNDI YALIYO PEMBEZONI 


22 Oktoba 2022.

Mtandao wa Jinsia Tanzania, tunatoa pongezi za dhati kwa mapendekezo yaliyotolewa na Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais kwa lengo la kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini. 

Kikosi kazi hiki kupitia Mwenyekiti wake, Prof. Rwekaza Mukandala, kimeweza kukabidhi taarifa yake kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yenye mapendekezo 18, ikiwemo mapendekezo yenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake na makundi yaliyo pembezoni katika uongozi na siasa. 


Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na 

Pendekezo la. 5: Katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi walau wajumbe wawili wawe wanawake, na sifa za kuwa Mwenyekiti, Makamu au Mjumbe ziainishwe. 

Pendekezo la 11: Sharti la uwepo wa Sera ya Jinsia kwenye Chama cha Siasa na ujumuishi wa makundi maalumu. Utararibu wa Viti maalumu uendelee ila sheria ziboreshwe na kuweka ukomo wa miaka 10 na pia, ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi usipungue asilimia 40. 

Pendekezo na. 12: sheria zinazo kwamisha ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye siasa ziangaliwe upya 

Pendekezo na. 13: juhudi za ushirikishwaji wa vijana kwenye siasa ziongezwe

Ni matumaini yetu kuwa mapendekezo haya yatachukuliwa na kutekelezwa kwa haraka ili kuweza kufikia malengo ya kuwa na demokrasia ya vyama vingi jumuishi na itakayoleta tija katika maendeleo ya taifa letu. 

Kipekee, tunatoa pongezi pia kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuwa sehemu ya mchakato huu kwenye kikosi kazi na kuweza kubeba na kuhakikisha ajenda ya masuala ya jinsia yanajitokeza katika mapendekezo hayo. 

Ikumbukwe kuwa, mnamo mwezi Februari mwaka huu, chini ya mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi unaotekelezwa na TGNP kwa kushirikiana na WiLDAF, tuliweza kufanya kikao cha mashuriano na Baraza la Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kikosi Kazi hiki cha Kuratibu maoni ya wadau kwa lengo la kuangalia mapengo ya kijinsia ndani ya vyama vya siasa na kukubaliana namna bora ya kuziba mapengo hayo ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi ndani na nje ya vyama vya siasa.  Miongoni mwa mapendekezo yaliyotoka katika kikao chicho cha mashauriano ni pamoja na uwepo wa Sera ya Jinsia katika vyama vya siasa. 

TGNP tunaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Baraza la Vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo hayo yaliyotolewa na kikosi kazi na kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunaweka misingi imara ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa siasa na ngazi za maamuzi.   Tunatambua mchango wa Kikosi Kazi, Baraza la vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kuleta mabadiliko na usawa wa kijinsia nchini. 


Tamko hili limetolewa na: 

Lilian Liundi 

Mkurungezi Mtendaji wa TGNP

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments