MMILIKI wa New Mwanza Hotel Mwita Gachuma amekanusha uvumi uliokuwa umesambazwa wa kuungua kwa eneo hilo lililoko katika mwa Jiji kwa kusema ni sehemu ya eneo hilo ndiyo ilipata tatizo hilo.
Amesema hayo leo jijini Mwanza kuwa ni sehemu ya eneo la nyuma ya hotel hiyo iliyokuwa inatumiwa kama ukumbi wa harusi na Kasino ambayo yameungua kwa moto unaohisiwa kutokana na hitilafu ya umeme.
Moto huo ulitokea usiku saa 1.30 siku ya tarehe 31 mwezi wa Nane kwa kile kinachohisiwa kuwa hitilafu ya umeme.
Gachuma ametoa shukurani kwa serikali ya mkoa huo, watendaji wa idara mbalimbali na wananchi kwa kuwezesha kuzimwa kwa moto huo kabla ya kuleta madhara makubwa kwa nyumba zilizopo karibu na sehemu hiyo.
Alisema madhara yaliyotokana na moto huo ni makubwa na watalaamu wa vyombo mbalimbali wamefika kufanya tathimini ya hasra hiyo kwani eneo hilo limeharibiwa vibaya na hivyo kuhitajika ujenzi upya.
"Watu wa Mamlaka Bima wamefika kwa ajili ya kufanya tathimini kuweza kujua ni kiasi gani cha hasara kimepatikana kutokana na moto huo hivyo siwezi kusema kiwango halisi cha hasara kilichopatikana" alisema Gachuma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima aliyefika tena kufatilia athari iliyotokana na moto huo alisema kuwa anashukuru vyombo vyote vya ulizi kwa kazi yao nzuri waliyofanya usiku wa tarehe 31 Agosti ilipoungua jengo hilo.
Alisema kutokana na jengo hilo kuwa katikati mwa majengo mengine madhara yake yangeweza kuwa makubwa zaidi endapo moto huo usingezibitiwa haraka.
'Nilikuwepo jana usiku kwenye tukio la moto huo hata hivyo nimeona nipite tena leo asubuhi kuona hali hiyo ambayo ingeweza kuleta madhara kwa moto huo kusambaa kwenye nyumba zingine' alisema Malima
Malima alitoa wito kwa watu wote kujenga majengo yao kwa kuweka tahadhari ya vitu vinavyozuia moto katika maeneo yao ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.