KARSAN ANG'ATUKA RASMI, MKURUGENZI MPYA WA UTPC KENNETH SIMBAYA AKABIDHIWA MIKOBA


Mkurugenzi mpya wa muungano wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Kenneth Simbaya (kulia), kushoto ni Rais wa Utpc Bw. Deogratius Nsokolo na katikati ni Bw. Abubakar Karsan Mkurugenzi ambaye amemaliza muda wake
Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC)  Deogratius Nsokolo amemkabidhi rasmi ofisi Bw. Kenneth Simbaya ambaye ni Mkurugenzi mpya wa UTPC. 

Bw. Simbaya anachukua nafasi ya Bw. Abubakar Karsan ambaye amemaliza muda wake.

Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 1/8/2022 katika ofisi za UTPC zilizopo Isamilo Jijini Mwanza ambapo Rais Nsokolo amesema UTPC ina matarajio makubwa kutoka kwa Bw. Simbaya na kwamba uzoefu wake kwenye kazi utasaidia kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa na mtangulizi wake na kuipeleka taasisi mbali zaidi.

Pamoja na mambo mengine Rais Nsokolo ametoa nasaha zake kwa mkurugenzi mpya, huku akigusia zaidi kuendeleza ushirikiano kati ya UTPC na wadau mbalimbali lakini pia kutumia fursa ya uwepo wa mkurugenzi aliyemaliza muda wake katika kubadilishana maarifa ya kiuongozi.

Pia amemtaka Bw. Simbaya kushirikiana na wafanyakazi wa UTPC, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na viongozi wa Klabu za waandishi wa habari katika utendaji wa kazi kwani anaamini ushirikishwaji huleta tija zaidi kwa maendeleo ya taasisi na kwamba taasisi haiwezi kuendeshwa na mawazo ya mtu mmoja.

Aidha amesisitiza kuhusu uadilifu na ubunifu katika utendaji wake wa kazi na kuimarisha ushirikiano na wafadhili ikiwemo kutafuta fursa mpya za kupata fedha. 

Hata hivyo alimdokeza kuhusu uwepo wa changamoto ndogondogo zilizopo katika klabu za waandishi wa habari licha ya jitihada zilizofanyika kutatua changamoto hizo.

"Uhai wa UTPC unategemea uwepo wa klabu za waandishi wa habari hivyo ni lazima tuhakikishe tunashirikiana kuzisimamia na kuzijengea uwezo klabu zetu'' ,amesema Rais Nsokolo.

Naye Mkurugenzi anayemaliza muda wake ndugu Abubakar Karsan ameeleza changamoto iliyokuwepo wakati anakabidhiwa nafasi ya ukurugenzi na kwamba hapakuwa na nyaraka zozote za makabidhiano hali iliyompa wakati mgumu katika kuifufua na kuiendeleza taasisi hiyo mpaka kuifikisha hapa ilipo leo.

"Nilikabidhiwa ukurugenzi hapa bila kuwa na nyaraka zozote, niliambiwa chukua kijiti nenda ukafufue taasisi" Karsan.

Hata hivyo Bw. Karsan ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mkurugenzi mpya kwa kipindi cha muda wa miezi mitatu ili kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na ndugu Kenneth Simbaya.

Kwa upande wake Bw. Kenneth Simbaya amesema nafasi ya ukurugenzi ni nafasi ambayo anaweza kupewa mtu yeyote hivyo ameahidi kuhakikisha anataguliza mbele maslahi ya waandishi wa habari na klabu zake na yale yote mazuri yatabaki kuwa mazuri kwa maslahi ya waandishi wa habari Tanzania.


Pia ameahidi kushirikiana na wafanyakazi pamoja na wadau wa UTPC katika kuhakikisha taasisi inasonga mbele "Maamuzi binafsi huyumbisha mwelekeo wa taasisi, hivyo niwahakikishe Bodi ya Wakurugenzi kwamba kila kitu kitaenda sawa kulingana taratibu zilizowekwa na kwa mujibu wa miongozo ya UTPC ", amesema Simbaya.

Aidha ameongeza kuwa kesho ya UTPC inategemea maamuzi mazuri yatakayofanywa leo, hivyo ili kuacha alama ni lazima kufanya kazi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu na kwa maslahi ya waandishi wa habari nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments