MWANAJESHI MSTAAFU AUA WAKIGOMBANIA MPAKA
MSTAAFU wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jonas Ziganyige (71), anashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumpiga risasi na kumuua mfanyabiashara, Patient Romward (48).

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam, Jumanne Muliro, amesema hayo jana na kuongeza kuwa baada ya tukio mtuhumiwa alikimbia, lakini alikamatwa eneo la Kibaha Maili Moja.

 Amesema mstaafu huyo mkazi wa Mbezi Juu, alifanya mauaji hayo, Julai 9,2022 saa 4 asubuhi, baada ya Patient ambaye ni mkazi wa Wazo Mivumoni, Kinondoni kufika eneo hilo kwa lengo la kukagua mipaka ya kiwanja chake.

Kamanda amesema marehemu alifika eneo hilo akiwa na mwenzie Recy Renso (52) na mtuhumiwa alitoka ndani huku akionesha kukasirishwa na hatua ya watu hao, akachukua bunduki na kumpiga risasi Romward. 

Amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alikimbia, lakini upelelezi umefanywa na Julai 10,2022 alikamatwa eneo la Kibaha Maili Moja akiwa amejificha.

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, pia limeipata silaha aliyotumia mtuhumiwa, ambayo ni aina ya Mark IV, ikiwa na risasi nne. 

Pia, katika tukio lingine jeshi hilo limewakamata watuhumiwa nane sugu wa matukio ya uvunjaji nyumba na kuiba vifaa vya magari, akiwemo Jumanne Omary (28), mkazi wa Mikwambe na wenzake saba wamekamatwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post