WATATU WAUAWA UGOMVI ENEO LA MALISHO YA MIFUKO TABORA


Watu watatu wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa wilayani Igunga mkoani Tabora katika mapigano ya kugombea maeneo ya kulishia mifugo.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao amesema tukio hilo lilitokea Mei 13, 2022 katika eneo la Isakamaliwa wilayani Igunga.

Amesema wananchi hao ambao walikuwa wanagombea maeneo ya kulishia mifugo, walitumia silaha za jadi kutekeleza mauaji hayo.

Kamanda Abwao amesema chanzo cha ugomvi huo ni kugombea sehemu ya kulishia mifugo na tayari msako wa kuwapata watuhumiwa wengine unaendelea baada ya watu wanne kukamatwa hadi jana kwa tuhuma za mauaji hayo.

Ameongeza kuwa matukio kama hayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu na kwamba ameagiza askari wake kuimarisha ulinzi wa usiku na mchana katika eneo hilo.

Kamanda Abwao amesema mtu mmoja aliyejeruhiwa katika tukio hilo anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Kamanda huyo amesema mkakati wa kumaliza mgogoro huo uliogharimu maisha ya watu umeanza kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo.


Chanzo:Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments