WATAALAMU WAPONGEZA JITIHADA ZA BENKI YA CRDB KUTOA ELIMU YA UWEKEZAJI


Benki ya CRDB imepongezwa kwa kuwa mstari wa Mbele katika kuelimisha Watanzania juu ya fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani na nje ya na namna ya kuzifikia. Pongezi hizo zimetolewa wakati wa Semina maalum ya Uwekezaji iliyoandaliwa na benki hiyo na kufanyika katika Makao Makuu yake mapya yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi Jijini Dar es Salaam, ambapo watu zaidi ya 5,000 walishiriki.

Akizungumza katika Semina hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji Kituo cha Wawekezaji Tanzania (TIC), John Mnali alisema jitihada zinazofanywa na Benki hiyo kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi zitasaidia kuongeza uelewa wa fursa za uwekezaji, kukuza idadi ya wawekezaji wazawa, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Tunafarijika kuona Benki yetu ya CRDB ipo mstari wa Mbele katika kushirikiana na Serikali kuwajengea wananchi uelewa juu ya fursa za uwekezaji. Pamoja na hivyo nimefurahishwa zaidi na utayari wao katika kutoa mitaji kwa wawekezaji wa ndani,” alisema Mnali.


Akielezea fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini, Mnali aliwataka Watanzania kutokaa nyuma katika kuchangamkia fursa za uwekezaji kwani Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji imekuwa ikitoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa.


“Kituo cha Uwekezaji sio tu kwa ajili ya wawekezaji wa nje, kinahudumia wawekezaji wote, kwa kutoa ushauri na kusaidia wawekezaji kufanikisha uwekezaji wao kwa kuwawezesha kupata vibali, leseni, na cheti cha uwekezaji,” alisema Mnali huku akitaka wananchi kizitumia vizuri pia taasisi zinazotoa huduma za uwekezaji kama ilivyo Benki ya CRDB.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya Semina hiyo ni kuona Watanzania wengi zaidi wanashiriki katika fursa za uwekezaji hapa nchini pamoja na kupata uelewa wa huduma za benki hiyo zitakazowasidia kuwa wawekezaji wazuri.


“Tumeona kazi nzuri inayofanywa na Serikali katika kuimarisha mazingira na kufungua milango ya fursa za uwekezaji. Tukiwa Benki kiongozi nchini ni wajibu wetu kuwaelimisha wananchi juu ya fursa hizi, lakini pia tumejipanga kuwawezesha kunufaika na fursa hzi kupitia bidhaa na huduma zetu bunifu,” alisema Nsekela.
Wataalamu na wabobevu wa uchumi na Uwekezaji kutoka Benki ya CRDB, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Kampuni ya Uwakala wa Hisa ya Orbit, Kampuni ya Bankable, Global Alliance, na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikuwepo kutoa madana kujadili fursa za uwekezaji na namna ya kuongeza ushiriki wa watanzania.


Baadhi ya fursa zilizojadiliwa ni pamoja na uwekezaji katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo, viwanda, nishati, usafirishaji, miundombinu, teknolojia, na Uwekezaji katika masoko ya mitaji ikiwamo Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Wataalamu hao walipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo wakibainisha kuwa changamoto kubwa inayosababisha ushiriki mdogo wa watanzania katika fursa za uwekezaji ni kukosa uelewa.
“Elimu kuhusu uwekezaji ndio imekuwa changamoto kubwa inayosababisha ushiriki mdogo wa Watanzania. Mfano katika soko la hisa Serikali imetoa vivutio vingi ambavyo vinamnufaisha mwekezaji lakini bado ni asilimia ndogo sana ya Watanzania wanashiriki katika Soko la Hisa,” alisema Ibrahimu Mshindo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara DSE.


Mshindo alibainisha changamoto hiyo imekuwa ikiwaogopesha wawekezaji wengi kutoka nje kuja kuwekeza nchini kwa kuona wazawa hawashiriki katika masoko ya mitaji kikamilifu. “Wawekezaji wengi hupenda kuwekeza katika nchi ambayo soko la hisa ni changamfu kwani wanajua pindi wanapotaka kutoka inakuwa rahisi kupata wawekezaji wapya ambao ni wazawa,” alisema.


Naye Dkt. Daniel Mushi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuna haja ya wananchi kuwekeza katika maarifa kwani kwa asilimia 80 ndio msingi wa kufanikiwa kwa uwekezaji wowote. “Watu wanadhani mtaji kwa ajili ya uwekezaji ni fedha tu au mitambo, hii inakamilisha asilimia 20 tu, asilimia 80 ya uwekezaji ni maarifa, kujua fursa ni ipi, na ufanyaje ili uwekezaji wako uwe na faida…”


“… na ndio maana mtu mwenye biashara iliyofanikiwa akifariki bila ya warithi kuwa na maarifa ya biashara, biashara hiyo hufa, kwasababu ameondoka na maarifa yake ya Uwekezaji,” alisema Dkt Mushi huku akisisitiza kuwa kuna haja ya Serikali na taasisi za fedha kuwashika mkono wawekezaji wadogo nchini na kuwaongoza katika fursa za Uwekezaji.

Washiriki wa Semina hiyo waliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo huku wakisema imesaidia sana kuongeza uelewa juu ya masuala ya uwekezaji na huduma za kifedha. Baadhi ya washiriki walipendekeza semina hiyo kufanyika hata mara tano kwa mwaka kwani bado uelewa wa masuala ya uwekezaji katika jamii ni mdogo.



Akitoa shukrani kwaniaba ya washiriki, Obeid Mwasajone ambaye pia ni Mwanahisa wa Benki ya CRDB aliishuru Bodi na Menejimenti ya benki hiyo kwa kuendelea kutekeleza programu za elimu ya uwekezaji na fedha kwa Watanzania. Alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania wengine kuwekeza katika Benki yao ya CRDB. “Faida ya kuwekeza huku ni kubwa mno, niwakaribishe mjionee wenyewe,” alisisitiza Mwasajone.
Mweneyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, akizungumza wakati akitoa shukrani kwa washiriki wa Semina maalum ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB, iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akizungumza wakati wa Semina maalum ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB, iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza wakati akiiongoza Semina maalum ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB na kufanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments