WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII YAANDAA MWAROBAINI KWA WANAOHARIBU MIMBA

 Waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu Dkt.Dorothy Gwajima akiongea na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita.


Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog- DODOMA


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amevitahadharisha vituo vinavyojihusisha na utoaji wa mimba huku akisema wizara yake inavifuatilia na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya vituo vitakavyobainika kufanya hivyo.


Akizungumzia mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan ,Dkt.Gwajima amesema,ni lazima serikali itachukua dhidi yao kwani kufanya hivyo ni kukatili uhai wa watoto waliotarajiwa kuzaliwa.


“Kuna taasisi fulani kazi yao ni kutoa mimba tutazifuatilia na tutachukua hatua za kisheria dhidi yao.”amesema Dkt.Gwajima


 Kuhusu mafanikio ya wizara hiyo Dkt.Gwajima amesema  ni pamoja na kuanzishwa kwa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) ambayo ni programu ya miaka mitano 2021/22-2025/26.


Amesema Wizara hiyo  imejenga Vituo Jumuishi vya Kijamii vya Kulelea Watoto (Community-Based Early Childhood Development Centers) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu hiyo.


“Vituo hivyo vina lengo la kutoa huduma jumuishi za Malezi na Makuzi kwa watoto walio na umri kuanzia miaka 2 hadi chini ya miaka 5  kwa kuwapatia huduma jumuishi za afya, lishe, ulinzi, ujifunzaji na uchangamshi wa awali kabla ya kujiunga na darasa la awali", amesema Dkt. Gwajima

Amesema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, jumla ya Vituo vya mfano 30 vimejengwa katika Mikoa ya Dar es Salaam vituo 10  na  Dodoma 20.

Kwa mujibu wa Waziri huyo , Wizara imeendelea kusimamia uanzishaji na uendeshaji wa huduma za vituo vya kulelea watoto wachanga na watoto wadogo mchana ambapo katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Wizara imesajili vituo 303 vilivyodahili watoto 6,772 (Me 3,194 na Ke 3,578).


Dkt. Gwajima amesema,vituo hivyo vinawezesha watoto kupatiwa huduma zinazochochea uchangamshi wa awali wa makuzi kimwili, kiakili, kihisia, kijamii na ukuaji wa lugha pamoja na kuwawezesha wazazi na walezi wa watoto kujihusisha na shughuli za kiuchumi wakati watoto wao wakiwa salama kituoni.


Akizungumzia kuhusu kuimarisha upatikanaji wa haki kwa watoto wanaokinzana na sheria sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu CCM Kifungu 93 (i) Serikali kupitia wizara hiyo imefanya ufuatiliaji  katika magereza yaliyopo mikoa ya Rukwa, Katavi, Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.


“Ufuatiliaji huu umewezesha watoto 16 kuachiwa huru kutoka Gereza Kuu la Segerea na kuwekwa chini ya uangalizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii, Jijini Dar es Salaam…,aidha, watoto watano wametolewa Gereza Kuu la Segerea na wamehamishiwa Mahabusu ya watoto Upanga,"amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments