KATAMBI : AMANI KUCHOCHEA FURSA ZA KAZI, AJIRA UMOJA WA AFRIKA KWA VIJANA WATANZANIA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, amesema, kutokana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan, kuendelea kuimarisha amani nchini, Mabalozi wa Vijana kwenye Umoja wa Afrika, Kitengo cha Amani na Ulinzi, wamepanga kushirikiana na Serikali katika masuala ya maendeleo ya vijana nchini. 

 Mhe. Katambi amefafanua kuwa Amani na Usalama ni msingi wa maendeleo, kwa kutambua kuwa mara nyingi vijana huusishwa na matukio ya ugaidi na uhalifu, hivyo mipango ambayo amejadiliana na mabalozi hao imejikita kwenye kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha vijana kwenye maendeleo ya kisiasa, kiutamaduni,  upatikanaji wa fursa za biashara, kilimo na uwekezaji.

Ameyasema hayo, jijini Dar es salaam, mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wawili wa Vijana kwenye, Umoja wa Afrika, Bi. Cynthia Chigwenya mwakilisha wa nchi 16 za ukanda wa Kusini mwa Afrika, pamoja na Bi. Diana Chando ambaye ni Mtanzania mwakilisha wa nchi 14 za ukanda wa Afrika Mashariki kwenye Umoja huo. 

“Huu utendaji ni maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa Ofisi yetu, baada ya mwaka mmoja wa uongozi wake, ametutaka vijana wawezeshwe. Tunataka kuwatumia mabalozi hawa wa vijana kwenye umoja huu, tupate fedha za kuweza kuwasaidia vijana kwenye fursa za ajira, kazi, mitaji, elimu, afya pamoja na maendeleo yao ya ustawi wa kiuchumi na kijamii” amesisitiza Katambi.

 Mhe. Katambi ameeleza kuwa ili vijana waweze kunufaika na fursa za umoja huo majadiliano hayo  yalijikita pia,  kwenye  athari za  mitandao ya kijamii  na Dawa za Kulevya kwa vijana, Upatikanaji wa up mikopo yenye riba nafuu kwa vijana, masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, magonjwa ambukizi pamoja na namna ya kuwajengea uzalendo vijana ili waendelee kuilinda amani.

Ameongeza kuwa katika eneo la Watu wenye Ulemavu ushirikiano wao utakuwa na tija kubwa kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye masuala ya Watu wenye Ulemavu kwani hadi sasa tayari imeandaa mwongozo wa kuwatambua mapema Wenye ulemavu ili waweze kuhudumiwa mapema.

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza mikataba ya Kimataifa na Kikanda na Protokali zinazoamuliwa katika maeneo mbalimbali hususani zinazohusika na Vijana, Kazi, ajira na Wenye  Ulemavu.

Kwa upande wake. Balozi wa Vijana kwenye Umoja wa Afrika, anayeshughulikia Amani, Bi. Cynthia Chigwenya ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuimarisha Amani nchini. 

Aidha, ameongeza kuwa amefurahishwa na jinsi Serikali inavyowapa nafasi vijana kwenye nafasi za kisiasa. Hivyo, amemhakikishia Mhe. Naibu Waziri kuwa watashirikiana kwenye fursa za maendeleo za umoja huo ili ziwanufaishe vijana wa Tanzania.

Naye, Balozi wa Vijana kwenye Umoja wa Afrika ambaye ni mwakilisha wa nchi 14 za ukanda wa Afrika Mashariki, Bi.Diana Chando, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwawezesha vijana ikiwemo kuwakopesha pamoja na kuwajengea uzalendo na kutambua umuhimu wa Amani. 

Amesisitiza kuwa uwepo wa Amani nchini unatoa uhakika wa shughuli za kisiasa na kiuchumi hivyo, itasaidia vijana kunufaika na fursa za umoja huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post