FAO, WADAU WA MIFUGO KANDA YA ZIWA WAKUTANA MWANZA KUFANYA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA YA TAIFA YA MIFUGO


Wa kwanza kushoto ni mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na uvuvi Dk. Heriel Massawe, (Katikati) ni Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Emil Kasagara, wakwanza kulia ni Dk, Moses Ole Neselle wakiwa katika picha ya pamoja kwenye kikao cha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006 kilichofanyika leo Mkoani Mwanza.


Na Hellen Mtereko, Mwanza

Shirika la Chakula na Kilimo(FAO) na wadau mbalimbali wa mifugo Kanda ya ziwa wamekutana Jijini Mwanza kwa lengo la kufanya mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006 ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa takribani miaka 15.


Kikao hicho kimefanyika leo Machi 1,2021 katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza


Akizungumza kwa niaba ya Katibu tawala Mkoa wa mwanza wakati wa kufungua kikao hicho, katibu tawala uchumi na uzalishaji Emil Kasagara amesema, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la Taifa kutoka wastani wa shilingi  Trilioni1 mwaka 2006/07 na kufikia wastani wa shilingi Trilion 10.6 mwaka 2020/21 ambapo kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya takwimu ya Taifa kwa mwaka 2021 pato la Taifa ni 148.5 Trilion.

Kasagara ameeleza kuwa kati ya mwaka 2006/07 na 2020/21 idadi ya mifugo imeongezeka kutoka ng'ombe milioni 18.5 hadi milioni 33.9, Mbuzi kutoka milioni 13.1 hadi milioni 24.5,kondoo kutoka milioni3.5 hadi milioni 8.5 huku kuku milioni 30 hadi milioni 87.7 jambo linaloonyesha mafanikio makubwa katika sekita ya ufugaji.


Pia ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya viwanda vya kusindika maziwa kutoka viwanda 22 mwaka 2005/06 hadi kufikia viwanda 105 mwaka 2020/2021 ambapo kwa Kanda ya ziwa tunajivunia kuwa na viwanda vikubwa vya kusindika mazao ya mifugo pamoja na machinjio ya kisasa katika maeneo mengi.


"Mafanikio hayo katika sekta ya mifugo yamechangia kuwainua Wananchi kiuchumi na kuchangia upatikanaji wa  malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo na kuwezesha biashara ya mifugo na mazao ya mifugo ndani nje ya Nchi hali itakayosaidia kuboresha lishe katika familia", amesema Kasagara.

Amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo pia kunachangamoto mbalimbali zinazoikakabili sekta ya mifugo ikiwa ni, kasi ndogo ya wafugaji kupokea na kutumia teknolojia  bora za uzalishaji mifugo zinazoendana na wakati ili kuongeza tija, uwepo wa magonjwa ya mifugo yanayoathiri uzalishaji na biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya Nchi, uwepo wa mbari za mifugo ya asili  zenye tija ndogo katika uzalishaji wa mazao ya mifugo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na uvuvi, Dk. Heriel Massawe amesema kuwa kikao hicho kimeshirikisha wadau kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera,Mara,Simiyu na  Shinyanga ili waweze kutoa maoni yao na uzoefu katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006.

"Kupitia kikao hiki wadau wa sekta ya mifugo watapata nafasi ya kutoa uzoefu wao katika utekelezaji wa sera iliyopo, sanjari na kuainisha changamoto za kisera wanazokutana nazo kutokana na mabadiliko yaliyojitikeza kati ya mwaka 2006 na 2021 ili waone namna ya kutatua changamoto hizo kupitia marekebisho ya sera",amesema Massawe.

Amesema kuwa katika kufanikisha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006, shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa(FAO) limeonyesha ushirikiano mkubwa kwa wizara kwa kutoa msaada wa kifedha ili kuweza kufanikisha zoezi hilo.

Dkt, Moses Ole Neselle ni mtaalam wa mnyororo wa thamani wa mifugo kutoka Shirika la chakula na kilimo (FAO) amesema kipaumbele chao ni kufanya kazi na Serikali katika maeneo mawili  ambayo ni Kilimo,mifugo ambapo watashirikiana bega kwa bega hadi pale watakapopata sera nzuri.

Mwenyekiti wa chama cha wafugaji Kanda ya ziwa,Charles Bwanakunu ambaye pia ni mmoja wa wadau walio shiriki katika kikao amesema kuwa ni muda sasa wa Serikali kuweza kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya mifugo ili wafugaji waanze kufuga ufugaji wenye tija na  waondokane na ufugaji wa asili ambao umekuwa  ukiwarudisha nyuma kiuchumi.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na uvuvi, Dkt. Heriel Massawe akizungumza katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo kilichofanyika leo Jijini Mwanza
Mtaalam wa mnyororo wa thamani wa mifugo kutoka Shirika la chakula na kilimo (FAO) Dkt. Moses Ole Neselle  akizungumza kwenye kikao cha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006
Wadau wa mifugo wakiwa kwenye kikao katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza
Wadau wa mifugo kutoka Mara wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi katika kikao kilichofanyika leo Jijini Mwanza katika ukumbi wa Gold Crest Jijini Mwanza
Wadau wa sekta ya mifugo kutoka Geita wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006
Wadau wa sekta ya mifugo kutoka Mkoa wa Mwanza wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi, katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments