MCHENGERWA AWAALIKA WANANCHI TAMASHA LA SERENGETI


*********

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwenye tamasha kubwa Tanzania na Afrika la Muziki la Serengeti (Serengeti Music Festival) litakalofanyika Machi 12, 2022 jijini Dodoma ili kujionea hazina ya vipaji vya wasanii nchini.

Mhe. Mchengerwa amesema haya, hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo amefafanua kuwa tamasha hili ndiyo tamasha kubwa linaloratibiwa na Serikali likiwa na lengo la kuibua vipaji vya wasanii pia kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuliingizia taifa mapato kutokana na hazina ya utalii uliopo.

Aidha, amesema tamasha hilo litahusisha wasanii zaidi ya hamsini wa miziki ya aina mbalimbali ambao watatumbuiza ili kuleta vionjo na radha tofauti tofauti.

“Tamasha hili linaleta muunganiko wa kipekee kabisa linaloonyesha tasnia ya burudani na utalii na ndiyo maana tumetumia jina la Mbuga yetu bora Afrika na duniani ya Serengeti ili kuwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani” amefafanua Mhe Waziri.

Amesema tofauti na matamasha mengine yote yanayofanyika nchini, tamasha hili linakwenda kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wanamuziki wa aina zote bila kujali lebo zao.

Ametoa wito kwa wasanii ambao watapata fursa ya kuimba, kujiandaa kikamilifu ili lengo la tamasha hili liweze kufikiwa.

Pia amesema wasanii na wanamuziki wakongwe wa zamani watapewa nafasi ili kuweza kurithisha kwa vijana wasanii wa muzikin wa kizazi kipya.

Amesema mtazamo wa Serikali kwa sasa ni kuwatafuta na kuwashirikisha wasanii kuanzia kwenye ngazi ya mtaa, vijiji, wilaya, mkoa hadi taifa ili wasanii waweze kuibuliwa na kuendelezwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments