SERIKALI YAYAFUNGULIA MAGAZETI YA MWANAHALISI, MAWIO, MSETO NA TANZANIA DAIMASerikali imeyafungulia rasmi magazeti ya Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima yaliyokuwa yamefungiwa kwa muda mrefu.

Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni ya magazeti hayo.

"Agizo la Rais ni sheria na inapaswa kutekelezwa Leo hii natoa Leseni kwa Magazeti manne ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima kwasababu ni vizuri kuondoka kwenye maneno tufanye vitendo hivyo tuanze na ukurasa upya sasa mwenye maneno yake aseme mwenyewe, kifungo kimetosha kikubwa kazi iendelee" , amesema  Nape Nnauye.

Akizungumza mara baada ya kupokea leseni za magazeti yake ambayo ni Mwanahalisi na Mseto, Said Kubenea ambaye ni mmiliki wa magazeti hayo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu kwa kufungua ukurasa mpya na vyombo hivyo vya habari huku akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali.

Uamuzi wa kufungulia magazeti hayo ni kutekeleza maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa Aprili 6, 2021 wakati akihutubia na kusema vyombo vya habari vilivyofungiwa, viongozi wa Serikali wenye dhamana waangalie namna ya kuvifungulia ili vifanye shughuli zake kwa kuzingatia sheria za nchi.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alimuomba Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuyafungulia magazeti yaliyofungiwa ya MwanaHALISI, Tanzania Daima, Mseto na Mawio, “Rais aliagiza vyombo vilivyofungiwa vifunguliwe. Tunakuomba sana, heshima ya Tanzania imeharibika, tuvifungulie.”

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments