AUAWA KWA KUCHOMWA KISU KWENYE MKUTANO WA CHAMA CHA CCC

Mtu mmoja ameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika mapigano kwenye mkutano wa chama cha upinzani huko Kwekwe, katikati mwa Zimbabwe, Jumapili.

Wafuasi wa Chama cha Wananchi (CCC) walivamiwa na kundi la watu waliokuwa na mikuki, mapanga, chuma na mawe.

Mtu mmoja aliuawa kwa kuchomwa kisu, wengine kuvunjika mifupa na majeraha mbalimbali, kwa mujibu wa maafisa wa chama.

Ghasia hizo zilimlazimu kiongozi wa chama Nelson Chamisa kuacha hotuba yake.

Chama hicho kiliwalaumu wafuasi wa Rais Emmerson Mnangagwa kwa ghasia hizo, madai ambayo chama tawala kilikataa.

Haya yanajiri huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionya kuhusu kuongezeka kwa ghasia kabla ya uchaguzi muhimu mdogo uliopangwa kufanyika tarehe 26 Machi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuhusu lugha za uchochezi katika kampeni hizo.

Mwishoni mwa juma makamu wa rais wa nchi hiyo alionya kwamba upinzani ungekandamizwa kama chawa, na hivyo kuzua hofu ya ghasia mpya.

Siku ya Jumamosi polisi walitumia vitoa machozi na maji ya kuwasha kutawanya mkutano mwingine wa CCC ambao ulikuwa umeidhinishwa na Mahakama Kuu.

Baadhi ya viti 28 vya ubunge na 122 vya udiwani vinawaniwa. Uchaguzi huo mdogo unaonekana kuwa mtihani kwa chama tawala cha Zanu-PF kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika 2023.

Kipindi cha kabla ya uchaguzi tayari kimekumbwa na madai ya hitilafu katika orodha ya wapigakura, ya upendeleo wa polisi na vyombo vya habari.

Chanzo- BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments