MGEJA AWATAKA WATANZANIA KUWA NA MAPENZI YA NJIWA KUKOMESHA MAUAJI


Ndege aina ya njiwa wakifurahia huku wakiwa wamemzunguka Khamis Mgeja, nyumbani kwake huku wengine baadhi wakiwa katika viganja vyake vya mikono ambapo ameeleza laiti kama Watanzania watakuwa na upendo kama wa ndege hao ni wazi mauaji ya watu yatakoma. Ndege hao wamekuwa na kawaida ya kumtembelea nyumbani kwake kila siku asubuhi, kutokana na upendo anaouonesha kwao.
Picha zote na Baltazar Mashaka
Mwanasiasa mkongwe nchini Khamis Mgeja,akiwa amezungukwa na ndege aina ya njiwa nyumbani kwake wilayani Kahama kama walivyokutwa na mpiga picha wetu.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja akiwa amezungukwa na ndege aina ya njiwa kwenye makazi yake wilayani Kahama, katika Mkoa wa Shinyanga.
Baadhi ya njiwa wakiwa wametua viganjani mwa Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja,wakidonoa chakula ambao ndege hao wamekuwa na kawaida ya kumtembelea nyumbani kwake kila siku asubuhi, kutokana na upendo anaouonesha kwao.

***


Na Baltazar Mashaka - Shinyanga
MAUAJI ya watu yanayotajwa kutokea maeneo mbalimbali nchini yanadaiwa kusababishwa na kukosekana kwa upendo,mshikamano na hofu ya Mungu miongoni mwa Watanzania na kuwataka kuonyesha mapenzi ya mfano wa njiwa (ndege) ili kukomesha vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation,Khamis Mgeja alisema jana katika mazungumzo na waandishi wa habari kuhusiana na ongezeko la matukio ya mauaji ya watu hivi karibuni katika maeneo mengi hapa nchini.

Alisema kukosekana kwa upendo,mshikamano na hofu ya Mungu miongoni mwa jamii ya Watanzania ni moja ya vyanzo vya mauaji ya watu huku mauaji hayo yakihusishwa na kuwania mali (kugombea mali) na wivu wa mapenzi na ili kuepuka mauaji ya aina hiyo watu bila kujali itikadi za kiimani na makabila yao wamrejee Mungu .

“Ukichunguza kwa undani ni wazi mauaji hayo yanayoripotiwa maeneo mbalimbali nchini yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na watu kutokuwa na upendo miongoni mwao,watu kukosa hofu ya Mungu hasa ikizingatiwa wanaofanya mauaji hayo baadhi ni watu wa karibu ndani ya familia ambapo baadhi ya watoto wanawaua wazazi wao kwa lengo la kupata mali,”alisema Mgeja.

Alisema endapo Watanzania watadumisha upendo na mshikamano miongoni mwao na kujenga hofu ya Mungu kama walivyo viumbe wengine mfano wa ndege aina ya njiwa itasaidia kupunguza matukio ya mauaji yanayotokea nchini au yasingekuwepo.


“Watanzania tudumishe upendo kama walivyo ndege aina ya Njiwa na viumbe wengine,bila upendo ni wazi tutaendelea kutoana roho kwa mambo madogo madogo ambayo kama mtu una hofu ya Mungu,upendo na mshikamano huwezi kufanya mauaji ya binadamu mwenzako,” alisema.

Mgeja alitoa mfano wake yeye mwenyewe amekuwa na tabia ya kuwakirimu njiwa (ndege) kwa kuwapa chakula na wao wameonesha upendo kwake ambapo kila siku asubuhi ndege hao hutua nyumbani kwake na kukaa naye ingawa wao si binadamu.

“Ukiacha wanadamu hata kama tutawakirimu viumbe wengine kwa kuwapa sadaka na kuwafanyia hisani, kuwahurumia na kuwathamini na wao pia wana nafasi kubwa ya kutuombea mbele ya muumba wetu ili tuishi kwa amani na upendo,” alisema Mgeja na kuongeza;

“Hali ya upendo ikidumishwa miongoni mwetu na kujenga utamaduni wa kuhurumiana sisi kwa sisi nchi yetu ama miji yetu itadumu kwenye amani na upendo, mfano ni hawa njiwa, mimi siwafugi,lakini huja hapa kila siku asubuhi, kisha wanaondoka, hii wanaonesha jinsi gani binadamu tunapaswa kupendana”,alisema.

Mwenyekiti huyo wa Tanzania Mzalendo Foundation,aliwaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini katika ibada na maombi yao ya kila siku wahimize sana suala la waumini wao kuwa na upendo na waone madhara ya kuuana wao kwa wao kwa mambo madogo madogo ya kidunia kwa vile duniani hapa ni mapito tu.

“Niwaombe Watanzania wenzangu,tumrejee muumba wetu bila kujali tofauti zetu za kidini,ukabila,kisiasa ama kijinsia, tukumbuke sisi sote ni ndugu, hatuna sababu za kuuana kwa suala la kutaka urithi ama wivu wa kimapenzi,tuisaidie serikali yetu kwa kuishi kwa amani na upendo ili tupate maendeleo,” alieleza Mgeja.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga na mwanasiasa mkongwe alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania kujenga utamaduni wa kupendana na kuhurumiana pale mmoja anapopatwa na matatizo asaidiwe badala ya kuchekwa,kama ni suala la mahusiano ya kimapenzi,busara itumike katika kutatua changamoto zinazojitokeza, badala ya kukimbilia kutoana roho.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments