WATAALAMU 422 WA TANZANIA BARA, ZANZIBAR WAPATIWA MAFUNZO YA ANWANI ZA MAKAZI


Muonekano picha ya vongozi na wataalam waliopo kwenye vituo vinne vya mikoa ya Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo ya anwani za makazi na postikodi kwa wataalam hao kwa njia ya mkutano mtandao wakati akiwa ofisi za TTCL, jijini Dodoma
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dorosela Rugaiyamu akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wataalam wa Halmashauri mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar wakati Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi (aliyeketi kulia)  akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu kwa ajili ya kutekeleza anwani za makazi katika mkutano uliofanyika leo ofisi za TTCL, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wataalam kutoka Halmashauri mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu hao  ya utekelezaji wa anwani za makazi katika mkutano uliofanyika leo ofisi za TTCL, jijini Dodoma.

***
 
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog, DODOMA.
KATIBU  Mkuu , Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amefunga mafunzo ya utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi huku akiwataka wataalamu hao kwenda kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuweka namba za nyumba, majina ya mitaa na barabara kwenye halmashauri wanazotoka.

Dkt.Yonazi amezungumza hayo leo Jijini Dodoma kwenye  mkutano baina yake na wataalamu hao uliofanyika kwa njia ya mtandao(video conference) yaliyofanyika kwenye vituo vinne vya mkoa wa Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar na kuongeza kuwa zoezi hilo kinapaswa kutekelezwa nchi nzima na kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi utasaidia kufungua kasi ya uchumi, utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi na kuifungua Tanzania kidijitali.

"Mkafanye kazi kwa ufanisi,ikiwa zoezi hili litafanikiwa mwananchi yeyote atatambulika duniani na anaweza kufikiwa na mteja kwa ajili ya kuuza bidhaa au huduma, hivyo kila mwananchi awiwe kuwa na namba ya nyumba, jina la barabara au mtaa anapoishi,” amesema 
 
Mbali na hayo  ametoa wito kwa kampuni, wadau mbali mbali na familia kuchangia utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi na kila mmoja awe balozi wa anwani za makazi na wataalam watoe taarifa kwa viongozi wao na Wizara iko tayari kuendelea kushirikiana kutekeleza hili
 
Kwa upande wake  Mratibu wa Kitaifa wa Anwani za Makazi na Postikodi wa Wizara hiyo, Mhandisi Jampyion Mbugi, amesema kuwa wataalam waliopatiwa mafunzo hayo ni wataalam wawili kutoka kwenye kila halmashauri nchi nzima ambapo inahusisha wataalam wa TEHAMA, Ardhi, Mipango Miji na Ramani.

Amesema, wataalamu hao wamepatiwa mafunzo hayo kwa muda wa wiki moja
kuanzia  Januari 17 hadi Januari 23 mwaka huu yanayolenga  utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi ikiwemo kuweka namba za nyumba, jina la mtaa au barabara na kuweka taarifa za maeneo hayo kwenye mfumo wa kielektroniki wa NAPA .

"Jambo hili ni muhimu sana kwa kuwa litawezesha  wananchi  kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta na kutunza muda ,"amefafanua.
 
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wataalam wengine waliopatiwa mafunzo hayo, Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Kilindi, Tanga ndugu Anastius Biswalo Manumbu amesema wamepatiwa mafunzo hayo kwa vitendo na wataenda kuwafundisha wataalam wengine ili kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinakamilika kwa wakati kuendana na azma ya Serikali .

"Tunawashukuru sana wawezeshaji kwani  tumeiva na sasa tupo tayari kutimiza wajibu wetu kwa vitendo na tutazingatia miongozo iliyopo ya uwekaji wa anwani za makazi na postikodi,"ameeleza.
 
Ufungaji huo wa mafunzo ya anwani za makazi na postikodi nchini, umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vituo vinne ambapo mafunzo hayo yametolewa kwa kuwashirikisha  wawakilishi wa wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa mikoa ya Tanga, Mwanza, Mbeya na Zazibar ambapo kwa upande wa Zanzibar waliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ndugu Amour Bakari

Aidha katika mafunzo hayo  jumla ya wataalam  422 wamepatiwa mafunzo ambapo wataalam 389 wametoka Tanzania Bara na 33 wametoka Zanzibar .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments