JESHI LA POLISI LASEMA ASKARI POLISI MAHEMBE ALIJIUA KWA KUJINYONGA


Gaitan Mahembe (kushoto), ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi anayedaiwa kujinyonga, Grayson Mahembe (kulia).
**

Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji zinazoendelea kuhusu tukio la kujinyonga hadi kufa kwa mkaguzi msaidizi wa jeshi hilo, Grayson Mahembe, tukio lililotokea Januari 22, 2022 mkoani Mtwara.

Taarifa iliyotolewa leo, Januari 31, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, SACP David Misime zinaeleza kwamba ushahidi ukiwemo wa picha na ripoti ya daktari, umethibitisha kwamba Mahembe alijiua kwa kujinyonga katika mahabusu ya peke yake aliyokuwa akishikiliwa kwa makosa yaliyokuwa yakimkabili yeye na wenzake.

Makosa hayo ni kudaiwa kushiriki kumnyang’amya fedha na kisha kumuua kijana aliyefahamika kwa jina la Mussa Hamis na kwenda kuutupa mwili wake vichakani katika Kijiji cha Namgogori mkoani Mtwara, tukio lililotokea Januari 5, mwaka huu.

Taarifa hiyo imeendelea kusisitiza kwamba wananchi hawapaswi kuamini taarifa za upotoshaji na mijadala inayoendelea na kuongeza kuwa askari huyo hakuzikwa kijeshi kwani kwa sheria za jeshi hilo, askari anapojitoa uhai, hawezi kupigiwa gwaride la mazishi linalochezwa na risasi au mabomu kwani anahesabiwa kuwa hajafa kishujaa.

Grayson Mahembe na wenzake saba, wanadaiwa kutekeleza mauaji ya kijana huyo Januari 5 mwaka huu na kisha mwili wa marehemu waliutupa katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Hiari wilayani Mtwara

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments