HII HAPA RATIBA YA MGAO WA UMEME


Wakati ratiba ya mgao wa umeme katika baadhi ya maeneo nchini wa siku kumi ikiwa haijatoka, wananchi, wakiwamo wafanyabiashara wadogo na sekta binafsi wanahofu shughuli zao kwenda mrama.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) juzi Ijumaa lilitangaza kuwapo maboresho ya vituo vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi l vinavyotegemewa kuzalisha megawati 185 na Ubungo lll megawati 112 kuwa vitasababisha mgao nchini.

Taarifa hiyo kwa umma inaeleza kuwa, upungufu huo wa umeme hautakuwa nchi nzima, isipokuwa kwa baadhi ya maeneo, lakini kila eneo litakaloathirika litapewa taarifa ni kwa muda gani kukosekana kwa umeme kutadumu.

“Lengo ni kuwawezesha wateja na wananchi kuweza kujipanga katika shughuli zao za kiuchumi na hata viwanda vikubwa vipange ratiba nzuri ya rasilimali watu kutokana na upatikanaji wa umeme,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande.

Pia, alisema Tanesco watatumia mwanya huo wa kukatika umeme kufanya matengenezo katika miundombinu ya usambazaji umeme, kwa kuwa kukatikakatika kwa huduma hiyo kunasababishwa na uchakavu.

Novemba 18, 2021 Tanesco ilitangaza kupungua kwa umeme, ikisema mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa maji katika vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa maji, hivyo kutakuwa na upungufu wa megawati 345.

Ilisema inachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kwa kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo ya Ubungo I inayozalisha megawati 25, ikisema itaendelea kutumia na vyanzo vingine mbadala kuhakikisha nishati hiyo inapatikana muda wote.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments